SIMBA NA MAANDALIZI YA CHINI YA MTI KUWAKABILI WAANGOLA
SIMBA SC |
Kuna eneo linaitwa Gymkhana,lipo Jijini Dar-es-Salaam. Wanamichezo wengi wa mkoa huo watakua wamewahi kufanya mazoezi kwenye eneo hili lenye viwanja vya michezo mbalimbali.
Ni eneo lenye miti mingi na utulivu wa kutosha tu. Lakini chini ya mmoja kati ya miti mikubwa ya eneo hilo kuna familia moja ya mama na watoto wake inafanya maisha yake hapo. Ni kitu cha ajabu lakini ni cha kweli.
Niliwahi kupiga stori na mama huyo, nikaiandikia makala mahali fulani na nikaipa kichwa cha habari 'MAISHA CHINI YA MTI'
Kikubwa nilichogundua ni kwamba mama huyo ana akili nyingi sana na anayaelewa maisha ipasavyo. Anajua kulea watoto wake na umri wake pia unamtosha. Swali nililobaki nalo ni, "Kwa nini bado anaishi chini ya mti wakati anaongea maneno yanayoashiria utajiri wa mawazo?"
Nilishasahau hii stori lakini nimekumbushwa na Simba. Simba hawa hawa 'Wekundu wa Msimbazi'.
Februari 17,2013 Simba wataiwakilisha Tanzania katika mchezo wa klabu bingwa barani Afrika dhidi ya Recreativo do Libolo ya Angola.
Ratiba ya michuano hii ilitoka siku nyingi sana,ilikua ni swala la kuuingiza mchezo huu kwenye mipango ya timu. Bahati nzuri ni kua ligi kuu ya Vodacom inaendelea hivyo ushiriki wa Simba ungeipa utayari wa kuliwakilisha taifa.
Kikosi cha Simba kina wachezaji wazuri sana kama akina Ramadhan Singano,Shomari Kapombe,Edward Christopher,Jonas Mkude na Haruna Chanonga. Hii ni nuru kwa taifa zima kwa ujumla.
Wakichanganywa na wazoefu wa michezo ya kimataifa kama akina Juma Kaseja,Amri Kiemba,Haruna Moshi na Mrisho Ngassa wangeweza kufanya vizuri kwa sharti moja tu, maandalizi mazuri.
Maandalizi yanayomaanisha soka pamoja na kujenga umoja wa timu, ukiongeza na uzalendo unaweza kujikuta unaitia aibu timu yoyote ile duniani. Lakini siyo maandalizi haya wanayoyafanya Simba.
Unalielewa vizuri benchi la ufundi la Simba?
Kuna kocha mkuu anaitwa Patrick Leiwing, kuna kocha msaidizi Moses Basena, Kuna kocha msaidizi Mwingine anaitwa Jamhuri Kihwelo 'Julio' na sasa kuna mdau wa siku nyingi anaitwa Talib Hilal ameongezeka hivi karibuni.
Hili ni jopo ambalo mgawanyo wake wa kazi unahitaji Diclopa kuuelewa. Na hapo ndipo ninapoifananisha Simba na yule mama anayeishi chini ya mti wakati ana akili nyingi kichwani mwake.
Wakati wa kuleta utulivu kwenye timu ndiyo wakati unaotumiwa na viongozi wa Simba kuongeza mikanganyiko kwa wachezaji aidha kwa kujua au kutojua,kupenda au kutopenda.
Nashindwa kuelewa nafasi ya kocha mkuu wa Simba ni ipi. Ninachokijua ni kuwa kocha mkuu ndiye bosi wa wachezaji na benchi la ufundi na yeye ndo hupanga mifumo ya uchezaji na yeye ndo huamua ni nani ataongea na wachezaji kama kuna umuhimu huo.
Simba wana kamati ya ufundi inayoongozwa na Ibrahim Masoud 'Maestro'. Kamati hii inayopaswa kuwa chini ya kocha na kutekeleza anachotaka. Sidhani kama Leiwing amemwita Talib kuja kuongeza nguvu Simba. Lakini hana jinsi,nae anapalilia kibarua chake. Unadhani hawa wazungu wanakuja hapa bila kutuelewa? Wanaokuja bila kutuelewa huwa hawadumu.
Afisa habari wa klabu ya Simba Ezikiel Kamwaga anasema "Talib hajaja kuchukua nafasi ya mtu Simba,amekuja kama mdau ambaye mchango wake unahitajika Simba".
Kamwaga anamalizia kwa kuwaomba waandishi wa habari kuacha kuandika habari zinazohusu migogoro isiyokuwepo ndani ya Simba kwa sababu Simba inawakilisha Taifa.
Taarifa hii ukiichunguza vizuri utagundua siyo Kamwaga wala mwanasimba yeyote anayefurahishwa na hali ya mambo klabuni hivi sasa lakini swali kwao linabaki kuwa ni kwa nini wanaendelea kuishi chini ya mti?
Kamwaga anasema hayo akijua kwamba kuna taarifa za Mrisho Ngassa kusemekana kwamba siku hizi haitumikii Simba ipasavyo kutokana na tetesi kuwa amesaini Yanga. Hizi siyo taarifa nzuri kwa sasa.
Kamwaga anasema hayo akijua pia kuna taarifa za Talib Hilal kupigiwa chapuo na Malkia Wa Nyuki ili aingie kwenye benchi la ufundi la Simba. Hizi pia siyo taarifa nzuri kwa sasa.
Kamwaga anaelewa pia kua Amir Maftah ana matatizo na uongozi wa Simba na ndiyo maana amekuwa haitumikii klabu hiyo kwa siku za karibuni.
Lakini hayo yote na mengine mengi, yasemwe au yasisemwe, haibadilishi kitu kwamba Simba wanafanya mzaha. Mzaha ambao matokeo yake ni migogoro isiyokuwa na tija.
Naona kama michuano ya klabu bingwa ni mzigo mzito kwa Simba msimu huu na wanatamani kuutua mapema ili waendelee kuishi chini ya mti.
Kumleta 'Malkia Wa Nyuki' ili awatangazie wachezaji utajiri wake,siyo maandalizi ya mpira. Maandalizi ya Mpira ni kama wanayofanya Azam FC ambao mpaka hivi sasa wanaonekana hata kwa macho tu kwamba wako tayari kushiriki kwenye kombe la shirikisho.
Sisi ngoja tuendelee kuwadai Yanga magoli yetu matano, tunajua hawalipi leo.
Imeandikwa na Richard Leonce Chardboy kutoka Wapenda Soka 'kandanda' group.
Nipate katika chardboy77@yahoo.com au 0658399341.
No comments