KAMUSOKO: TUPO TAYARI KUTWAA KOMBE LA SPORTPESA
Nahodha wa klabu ya Yanga, Thaban Kamusoko anaamini kuwa timu yao ipo tayari
kwa ajili ya michuano ya SportPesa Super Cup inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi
siku ya Jumapili ya Juni 3 jijini Nakuru.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa
mazoezi ya jioni yaliyofanyika kwenye viwanja vya Nakuru Athletic Club,
Kamusoko amethibitisha kuwa kikosi cha Yanga kina morali ya kutosha kwa ajili
ya kuwavaa wapinzani wao Kakamega Homeboys kwenye mechi ya ufunguzi.
“Timu ipo vizuri na ina morali ya
hali ya juu kuelekea kwenye mchezo wetu wa kwanza na hakika tumedhamiria
kufanya makubwa kwenye michuano hii kwani ukweli ni kuwa Yanga ni timu kubwa na
inacheza ili kushinda mataji.
Nahodha huyo anayekaimu nafasi ya
nahodha mkuu, Nadir Haroub amesema wataingia kwenye mchezo wao wa ufunguzi kwa
kujiamini licha ya kutowajua wapinzani wao vyema.
“Hatuwajui sana wapinzani wetu lakini
naamini wao wanatujua kwasababu Yanga ni klabu kubwa na tunacheza mashindano ya
kimataifa kila mwaka lakini sisi hatuwafahamu wao kiundani kwasababu hatujawahi
kuwasikia”, alisema.
Akizungumzia michuano iliyopita
ambayo Yanga ilitolewa kwenye hatua ya nusu fainali na AFC Leopards ya Kenya,
Kamusoko amesema safari hii Yanga imeenda Kenya wakiwa kamili ili waweze kurekebisha
makosa yao
![]() |
Nahodha wa Yanga katika mIchuano ya Sportpesa |
“Mwaka jana hatukutilia maanani michuano hii lakini tulikuja kujua umuhimu wake baada ya Gor Mahia kucheza na Everton kwa hiyo mwaka huu tumejipanga kuhakikisha haturudii makosa yaliyojitokeza”, alisisitiza Kamusoko.
Naye kocha msaidizi wa kikosi hicho
cha mabingwa mara 27 wa Tanzania Bara, Noel Mwandila amesema watafanya kila
liwezekanalo kuhakikisha wanatwaa kombe hilo ili waweze kupata faraja baada ya
kushindwa kufurukuta kwenye ligi ya ndani.
“Tuna kila sababu ya kufanya vyema
kwenye michuano hii ili tuweze kuwapa faraja mashabiki wetu ambao wamekuwa
wakituunga mkono tangu mwanzo wa msimu”, alihitimisha.
Yanga itakata utepe wa michuano ya
SportPesa Super Cup siku ya Jumapili kwenye dimba la Afraha majira ya saa 7
kamili mchana kwa kuwavaa Kakamega Homeboys ambao wanashika nafasi ya tisa
kwenye msimamo wa Ligi Kuu nchini Kenya.
Timu itakayofanikiwa kushinda kwenye
mchezo huo wa ufunguzi itakutana na mshindi wa mechi kati ya Simba na
Kariobangi Sharks kwenye hatua ya nusu fainali.
No comments