AZAM: MECHI YA YANGA ITAKUWA FAINALI

Azam FC inaamini mchezo wao wa mwisho dhidi ya Yanga utakuwa mgumu kama fainali kwakua kila timu inahitaji kumaliza nafasi ya pili kwenye msimamo.

Azam imeizidi Yanga alama tatu lakini kama vijana hao wa Jangwani watashinda mechi hiyo itakayopigwa Jumatatu watashika nafasi ya pili kwa uwiano mzuri wa mabao.

Msemaji wa klabu ya Azam, Jaffer Idd amesema siku zote mechi dhidi yao na Yanga zinakuwa ngumu hata kama mmoja akiwa katika hali mbaya ya kiuchumi.

Jaffer amesema wanafahamu Yanga wanapitia kipindi kigumu na wamepoteza mechi nyingi mfululizo lakini haiwapi nguvu ya kusema watashinda mchezo huo.

"Mechi yetu dhidi ya Yanga itakuwa ni ya heshima kila timu inahitaji kumaliza nafasi ya pili, mchezo utakuwa mgumu na aliyejiandaa vizuri atapata ushindi.

"Tupo kambini muda mrefu kujiandaa na mchezo huu tunahitaji kushinda ili kumaliza nafasi ya pili kulinda heshima," alisema Jaffer.

Mchezo huo utaanza saa 2 usiku katika uwanja wa Taifa ili kuwapa nafasi Azam TV kuonyesha mechi nyingi kwakua itakuwa ni siku ya mwisho ya kukamilisha msimu.

No comments

Powered by Blogger.