KAGAME KUPIGWA DAR JUNI MWAKA HUU
Michuano ya klabu bingwa ya Afrika Mashariki na Kati
inayosimamiwa na Baraza la vyama vya soka ukanda huo (CECAFA) maarufu kama
Kagame Cup yanatarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam mwezi Juni mwaka huu.
Michuano hiyo inarejea baada ya kupita miaka mitatu
kufuatia kukosena kwa wadhamini huku bingwa mtetezi akiwa Azam FC.
CECAFA imepokea kiasi cha dola Milioni moja kutoka
Shirikisho la soka duniani (FIFA) ili kufanikisha mashindano mbalimbali
yakiwemo ya vijana chini ya umri wa 17 yatakayofanyika nchini Burundi, pamoja
yale ya Wanawake na Wanaume kwa nchi wanachama.
Taarifa za ndani kutoka katika uongozi wa CECAFA
zinasema kuwa michuano hiyo itafanyika kati ya Juni 30 hadi Julai 14 jijini Dar
badala ya Djibouti kama ilivyotangazwa awali.
Taarifa zimezidi kusema kuwa michuano hiyo ilipangwa
kufanyika nchini Djibouti lakini Azam TV ambao wameingia mkataba kurusha
matangazo hayo moja kwa moja wameshauri kubadilishwa kutokana na sababu za
kiusalama.
Simba ndio inaongoza kwa kutwaa taji hilo mara
nyingi ikifanya hivyo mara sita ikifuatiwa na Yanga na Gor Mahia zilizotwaa
mara tano.
No comments