CHIRWA AWATOLEA UVIVU MASHABIKI MTANDAONI

Mshambuliaji Obrey Chirwa wa Yanga amewatolea uvivu mashabiki wanaomzushia mitandaoni kuwa amegoma na kushindwa kusafiri kwenda Shelisheli.

Jumatano ya wiki hii Yanga itacheza mchezo wa maruadiano wa ligi ya mabingwa Afrika dhidi ya St Louis ya visiwani humo ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa bao moja iliyopata hapa nyumbani.

Chirwa amewafungukia mashabiki hao kwa kuwaambia hatima ya maisha yake ndani ya Yanga anajua mwenyewe na klabu hiyo.

"Sijawahi kusema wala kumwambia mtu kuwa nataka milioni 150 kwa ajili ya mkataba mpya, sipendezwi na namna wanavyonizushia nadhani nia yao ni kunigombanisha na wapenzi wa Yanga.

"Niliumia kwenye mchezo dhidi ya Majimaji ajabu wanasema nimegoma, huu ni upuunzi. Mimi ni mchezaji wa Yanga, mimi na klabu ndio wenye kujua hatima yangu ya baadae, niacheni nicheze mpira," alinukuliwa Chirwa.

Uvumi huo ulizagaa zaidi jana baada ya Chirwa kutokuwepo miongoni mwa wachezaji 20 wa Yanga waliosafiri kuelekea Shelisheli kwa mchezo huo.

No comments

Powered by Blogger.