YANGA NAO WAGEUKIA MABADILIKO MCHAKATO WA HISA KAMA SIMBA WAANZA

Mabingwa wa soka Tanzania bara Yanga wameanza mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshwaji wa klabu hiyo kongwe nchini kutoka katika umiliki wa sasa ambao unategemea wanachama kwenda katika mfumo wa uendeshaji wa Hisa ambao utakaribisha uwekezaji.

Akiongea jijini Dar es Salaam Katibu mkuu wa klabu hiyo Charles Boniface Mkwasa amesema Juzi tarehe 13 kamati ya Utendaji ya klabu hiyo ilikutana kujadili mambo mbalimbali yanayohusu klabu hiyo lakini kubwa kabisa likiwa ni mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji na sasa kinachosubiriwa ni mkutano mkuu wa wanachama utakaofanyika ndani ya miezi mitatu kubariki mabadiliko hayo.

Sambamba na kusubiri mkutano huo lakini pia kamati ya kuratibu mchakato huo itatangazwa hivi karibuni ili kuweza kutoa elimu ya mfumo huo mpya ambao utakuwa ni wa Hisa ambazo asilimia 51 itabaki kwa wanachama wakati asilimia 49 itaenda kwa wawekezaji.


Yanga inaingia katika mchakato huu ikiwa ni siku chache baada ya Waziri wa habari Mheshimiwa Harisson Mwakyembe kubariki mabadiliko ya mfumo yaliyofanywa na Simba Disemba 3 na kuwa klabu ya kwanza Afrika Mashariki kuingia katika mfumo huo ambapo Mohammed Dewji Mo alishinda zabuni ya umiliki wa klabu ya Simba.

No comments

Powered by Blogger.