MAN UNITED YAREJEA NA USHINDI LIGI YA MABINGWA ULAYA,POGBA AUMIA
Mabingwa wa Europa League msimu uliopita Klabu ya Manchester United Imerejea vyema kwenye ligi ya mabingwa Ulaya msimu huu ikiibuka na ushindi wa bao 3-0 kwenye mchezo wake dhidi ya FC Basel ya Uswisi.
Pambano hilo lililopigwa kwenye uwanja wa Old Trafford lilishuhudia Paul Pogba akiiongoza Man United kama nahodha baada ya Michael Carick na Antonio Valencia kuanzia benchi lakini Pogba hakudumu mpaka mwisho wa mchezo baada ya kuumia dakika ya 20 na nafasi yake kuchukuliwa na Maruane Fellaini.
Mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika United walikua mbele kwa bao 1-0 bao la Maroane Fellaini dakika ya 35 baada ya kuunganisha kwa kichwa mpira wa Ashley Young.
Kipindi cha pili United waliongeza bao la pili dakika ya 65 safari hii likifungwa na Romelu Lukaku akiunganisha kwa kichwa pia mpira wa kona iliyopigwa na Daley Blind wakati Marcus Rashford yeye alimaliza kazi akifunga bao la tatu baada ya kuingia kuchukua nafasi ya Juan Mata.
Mechi nyingine ya kundi hili la A ilishuhudiwa CSKA Moscow wakiwa ugenini wakiibuka na ushindi wa bao 2-1 dhidi ya wenyeji Benfica.


No comments