LIGI KUU TANZANIA BARA: SIMBA YAVUTWA SHARUBU NA MBAO FC
Mchezo wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya Mbao FC ya Mwanza na Simba ya Dar es Salaam umemalizika kwa timu hizo kugawana pointi baada ya sare ya mabao 2-2.
Wekundu wa Msimbazi, Simba walikua wa kwanza kuandika bao katika kipindi cha kwanza likifungwa kwa kichwa na Shiza Kichuya na kudumu hadi mapumziko.
Utamu wa mechi ulianza kipindi cha pili ambapo Mbao walisawazisha kupitia Haji Kiondo kwa shuti la mbali lililomshinda golikipa Aishi Manula.
Simba walijibu bao hilo dakika mbili baadae kwa kuandika bao la pili kupitia kwa James Kotei akiunganisha vizuri mpira wa faulo uliopigwa na Erasto Nyoni.
Wakati kila mtu akiamini kwamba Simba wataondoka na alama tatu katika mchezo huo, Boniface Maganga wa Mbao FC alipiga mpira akiwa nje ya eneo la hatari la Simba ambao ulikwenda moja kwa moja nyavuni na kuandika bao la pili.
Hadi dakika 90 zinamalizika, Mbao 2-2 Simba.
Huu ni mchezo wa kwanza kwa Simba kuruhusu bao katika ligi kuu ya Vodacom msimu huu.

No comments