KISA JEZI FEKI, SIMBA YAMWANGUKIA RC MAKONDA


Wekundu wa Msimbazi Simba wamemwangukia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mheshimiwa Paul Makonda ili awasaidie kupambana na wanaohujumu mapato ya klabu hiyo katika uuzaji wa jezi.

Mkuu wa Kitengo cha Habari wa klabu hiyo Bwana Haji Manara amemwomba Makonda leo katika kikao chake na Waaandishi wa Habari jijini Dar es Salaam na hii inatokana na Manara kudai kwamba watu wamekua wakitengeneza Jezi feki na kuziuza kinyume na utaratibu wa klabu hiyo ambao ulitangazwa awali sambamba na kuwatangaza mawakala.

Manara amemwomba mheshimiwa Makonda ambaye pia ni mwenyekiti wa Ulinzi na usalama wa mkoa kutumia vyombo vyake kuwakamata wale wote wanaojihusisha na biashara hiyo bila utaratibu kwakua Simba haina uwezo wa kuwakamata.

Katika hali nyingine Manara pia ametangaza kamati maalumu ya kuratibu mchakato wa kupata mwekezaji atakayenunua shea za klabu hiyo 50% kama ilivyopitishwa na mkutano mkuu wa wanachama kuelekea mabadiliko ndani ya klabu hiyo kongwe nchini.

Kamati itaongozwa na Jaji wa mahakama kuu Thomas Mihayo kama Mwenyekiti, Sambamba na wajumbe wanne ambao ni Idd Azan Zungu (MB), Ndugu Abdulrazaq Badru, Wakili Dkt Damas Ndumbaro na Ndugu Yusuph Maggid Nassoro.

Kamati hiyo itahusika na kusimamia taratibu zote za manunuzi kwa mujibu wa kanuni na sheria za nchi na makubaliano ya mkutano mkuu wa Simba wa tarehe 20 mwezi uliopita.

No comments

Powered by Blogger.