SPORTPESA YAINGIA AFRIKA KUSINI, YAMWAGA PESA KWA CAPE TOWN CITY FC


CAPE TOWN, Afrika Kusini - Klabu ya Cape Town City inayoshiriki Ligi Kuu ya nchini Afrika Kusini maarufu kama PSL imekuwa klabu ya kwanza kutoka nchini humo kudhaminiwa na kampuni ya michezo ya kubashiri ya SportPesa.

Klabu hiyo ambayo ilimaliza katika nafasi ya tatu ya msimamo wa Ligi wa Afrika Kusini kwa msimu uliopita wa 2016/17 imeingia kwenye makubaliano ya udhamini kwa mkataba wa rekodi wa miaka minne na SportPesa ambao ndio watakuwa wadhamini wao wakuu kwenye jezi zao pamoja na kuwa washirika rasmi wa klabu hiyo katika michezo ya kubashiri.

Mkurugenzi wa SportPesa Afrika Kusini, Nick Ferguson pamoja na Mmiliki wa klabu ya Cape Town, John Comitis walisaini makubaliano hayo jijini Cape Town siku ya ijumaa Agosti 11 huku magwiji hao wa michezo ya kubashiri duniani wakitambulisha uwepo wao kwenye Ligi hiyo ambayo inatajwa kuwa ligi tajiri zaidi barani Afrika.

“Tunawakaribisha washirika wetu wa kwanza nchini Afrika Kusini ambao ni
Cape Town City FC kwenye familia yetu ya SportPesa. Udhamini huu ni uthibitisho kutoka SportPesa kuwa tumejidhatiti katika kuhakikisha tunachangia maendeleo ya mpira wa miguu kwenye nchi hii.

“Tuna furaha kubwa sana kufanya kazi na Cape Town City FC, klabu ambayo inaendana na thamani yetu na tunatazamia kuwa na kipindi cha mafanikio ambacho kitahamasishwa na safari hii ambayo tumeianza pamoja”, alisema Ferguson wakati wa sherehe ya kutiliana saini.

Nembo ya SportPesa sasa itakuwa ikionekana upande wa mbele wa jezi rasmi ya Cape Town City FC baada ya timu hiyo kuingia kwenye orodha ya timu kubwa za mpira wa miguu duniani zinazodhaminiwa na kampuni hiyo. Makubaliano haya yanahusisha timu ya wakubwa, timu B na timu za vijana za Cape Town City, ambayo itashiriki kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho la Afrika kwa mawaka 2018 baada ya kumaliza nyuma Bidvest Wits na Mamelodi Sundowns kwenye msimamo wa Ligi ya Afrika Kusini
Klabu hiyo ilianzishwa na mfanyabiashara John Comitis ambaye ni mmiliki
wa zamani wa Cape Town Spurs na mwanzilishi wa Ajax Cape Town
mwaka 2016 ambapo ndipo Cape Town City FC ilizaliwa upya ikiwa ni
miongoni mwa vilabu vilivyotamba nchini Afrika Kusini katika miaka ya
1960 na 1970.

No comments

Powered by Blogger.