TAIFA STARS YAFIKA SALAMA, KUANZA NA MALAWI
Kikosi cha wachezaji 22 wa timu ya Tanzania ‘Taifa
Stars’, kimesafiri na kufika salama nchini Afrika Kusini kikitokea Dar es
Salaam, Tanzania.
Timu hiyo iliyoondoka Alhamisi Juni 22, 2017 kwenda Afrika Kusini kwa ndege ya Shirika la Ndege la
Rwanda, itakuwa huko kwa ajili ya michuano ya kuwania Kombe la Castle Cosafa.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Bia
ya Serengeti, itaanza kampeni za kucheza hatua ya Robo fainali kwa kucheza na
Malawi Jumapili, Juni 25, mwaka huu katika michuano hiyo iliyoandaliwa na
Baraza la Mpira wa Miguu la nchi za Kusini mwa Afrika (Cosafa).
Tanzania si mwanachama wa Cosafa,
lakini imealikwa katika mashindano hayo na imepangwa kundi A na timu za
Mauritius, Malawi na Angola wakati Kundi B ni Msumbiji, Shelisheli, Madagascar
na Zimbabwe. Kinara wa kila kundi atakwenda moja kwa moja hatua ya robo
fainali.
Timu za Botswana, Zambia na
Afrika Kusini kadhalika Namibia, Lesotho na Swaziland tayari zimepangwa hatua
ya robo fainali hivyo zinasubiri vinara wawili kutoka makundi ya A na B
kuungana nazo kucheza robo fainali.
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Salum
Shabani Mayanga, amesema kwamba anaichukulia michuano hiyo kwa umakini na uzito
mkubwa kwa wachezaji kuzidi kupata uzoefu wa mechi nyingi za kimataifa kwa
mwaka.
Kadhalika, kiufundi Mayanga
anachukulia michuano hiyo kama sehemu ya maandalizi makubwa ya mchezo dhidi ya
Rwanda wa kuwania kucheza nafasi ya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya
Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani - CHAN.

No comments