HIMID MCHEZAJI BORA WA MASHABIKI AZAM
Nahodha Msaidizi wa Klabu Bingwa
ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Himid Mao ‘Ninja’, amefanikiwa kuwa
Mchezaji Bora wa mashabiki wa timu hiyo msimu uliopita.
Ninja ameibuka kidedea baada ya
kupigiwa kura nyingi na mashabiki kwenye mitandao ya kijamii ya mabingwa hao
(facebook - Azam FC na instagram - azamfcofficial), akiwazidi nyota wengine
wawili wa timu hiyo, beki kisiki Yakubu Mohammed na mshambuliaji anayekuja kwa
kasi, Shaaban Idd.
Kwa mujibu wa takwimu za mchuano
huo, kura zote zilizofanya uamuzi huo kwa kukubaliwa zilikuwa 293, huku
ikishuhudiwa Ninja aliyekuwa kwenye kiwango bora kabisa msimu uliopita akizoa
zaidi ya nusu ya kura hizo ambazo ni 151.
Mohammed amefuatia katika nafasi
ya pili kwa kuvuna jumla ya kura 72 akimzidi kura mbili tu Shaaban aliyefunga
dimba baada ya kujikusanyia 70.
Mchakato wa kuwapata wachezaji
hao watatu walioingia kwenye kinyang’anyiro hicho uliwahusisha mashabiki katika
kurasa hizo za Azam FC ndani ya mitandao hiyo ya kijamii, ambao waliwachagua
kwa wingi kuwa wachezaji wa msimu wa timu hiyo.
Ninja ambaye hivi sasa ni Nahodha
Msaidizi wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, amerithi mikoba ya
aliyekuwa beki wa timu hiyo, Shomari Kapombe, aliyeitwaa mwaka jana mara baada
ya kumalizika kwa msimu wa 2015-2016.

No comments