AZAM FC YAANZA KUUVUTIA KASI MSIMU UJAO YAALIKWA RWANDA
KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki
na Kati, Azam FC, jana jioni imeanza rasmi mazoezi ya kujiandaa na msimu ujao
(2017-2018) huku ikiwa imepata mwaliko maalum nchini Rwanda kutoka kwa mabingwa
wa nchi hiyo, Rayon Sports.
Awali Azam FC ilipanga kuanza maandalizi ya
msimu mpya Jumatatu ijayo Julai 3, lakini kutokana na mwaliko huo imeamua
kuanza mazoezi mapema, ambapo Rayon imealika kwa ajili ya kucheza nao mchezo wa
kirafiki Julai 8 ikiwa ni sehemu ya kusherehesha ubingwa walioutwaa.
Wachezaji waliofanikiwa kuhudhuria kwenye
mazoezi hayo ya kwanza ni pamoja na makipa Mwadini Ally, Benedict Haule,
aliyerejea Azam FC kwenye usajili huu akitokea Mbao FC, Metacha Mnata na mabeki
Bruce Kangwa, Abbas Kapombe, Ramadhan Mohamed, Abdul Omary.
Viungo ni Frank Domayo, Masoud Abdallah,
Stanslaus Ladislaus na mshambuliaji Yahaya Zaidi, huku wachezaji wengine wakiwa
na udhuru na baadhi wakiwemo kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa
Stars’ kinachoshiriki michuano ya COSAFA, Nahodha Msaidizi Himid Mao ‘Ninja’,
beki Gadiel Michael, kiungo Salmin Hoza na mshambuliaji Mbaraka Yusuph.
Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Kocha
Msaidizi wa Azam FC, Idd Nassor Cheche, alisema kuwa mbali na mwaliko huo
kupelekea kuanza mapema mazoezi, pia sababu nyingine ni kuwaweka fiti zaidi
wachezaji ambao hawakuchaguliwa timu ya Taifa ili watakapoungana na wale
walioitwa waweze kwenda sawa.
“Tukapokwenda Rwanda kati ya tarehe 5 hadi 6,
tunaweza kupata siku kadhaa za kufanya maandalizi yetu pamoja na kucheza mechi
kadhaa kabla ya kurejea nyumbani tayari kabisa kufanya maandalizi ya mwisho kwa
ajili ya ligi ya msimu ujao,” alisema.
Cheche alisema amefurahishwa sana na namna
alivyowaona wachezaji kwenye mazoezi hayo ya kwanza huku akieleza kufurahishwa
na usajili unaoendelea kufanywa na timu hiyo mpaka sasa na sera ya klabu ya
kupandisha wachezaji kutoka Azam Academy.
“Maingizo ni mazuri na kilichobakia hivi sasa
ni kufanya mazoezi kwa pamoja na kuelewana na wenzao, wajuane kitabia nje na
ndani ya uwanja ili waweze kushirikiana ma kubwa kuweza kulisukuma mbele
gurudumu hili la Azam FC,” alisema.
Azam
FC inayodhaminiwa na Benki bora ya NMB na kinywaji safi cha Azam Cola,
itaendelea tena na mazoezi kesho saa 10 jioni.
No comments