SIMBA YALIPIZA KISASI KWA LYON YARUDI KILELENI VPL


Wekundu wa Msimbazi Simba wameweza kulipiza kisasi cha kufungwa na African Lyon Mzunguko wa kwanzavwa ligi kuu Tanzania bara kwa kuibuka na ushindi wa bao 2-1 leo.

Simba ilipata ushindi huo katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam mechi iliyoambatana na mvua kubwa iliyokua ikinyesha jijini Dar leo.

Mshambuliaji Ibrahim Ajibu alitangulia kuipatia Simba bao la kwanza dakika ya 37 baada ya kupiga shuti kali lililomparaza beki wa Lyon na kutinga wavuni.

Dakika moja kabla ya mapumziko Omary Abdallah aliweza kuifungia Lyon bao la kusawazisha akitumia makosa ya safu ya ulinzi ya Simba ambayo ilikua imepoteana na kufanya timu hizo kwenda mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1.

Kipindi cha pili mvua kubwa iliyokua ikinyesha iliharibu ladha ya mpira kutokana na wachezaji  kuanguka mara kwa mara na dakika ya 55 Hamad Wazir ambaye ni beki wa Lyon alijifunga wakati akijaribu kuokoa mpira uliopigwa na Mavugo.

Kwa matokeo hayo Simba inarudi Kileleni mwa msimamo wa ligi kwa sasa ikiwa na pointi 62 ikifatiwa na Yanga yenye pointi 59.

No comments

Powered by Blogger.