SERENGETI BOYS WAANZA NA SARE DHIDHI YA MABINGWA WATETEZI

Timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 18 imeanza kampeni yake yenye jina la Gabon Mpaka Kombe La Dunia leo katika michuano ya Afrika kwa vijana wenye umri huo kwa kuvaana na mabingwa watetezi Mali.

Wakiwa bila nahodha wao Issa Makamba ambaye ameondolewa kikosini baada ya kuvunjika kidole cha mguu wake, Serengeti Boys walifanikiwa kupata sare ya bila kufungana katika mchezo huo uliokua mgumu kwao.

Vijana wa Mali ambao wengi walionekana kuwa wazoefu kutokana na kucheza katika vilabu vya ligi kuu katika mataifa tofauti, walitawala sehemu kubwa ya mchezo hasa eneo la katikati lakini viungo wa Tanzania wakiongoza Ally Ng'azi walisimama imara katika eneo la kiungo.

Pamoja na kuonekana kuzidiwa, lakini vijana wa Tanzania hawakua nyuma katika kujaribu kutengeneza nafasi chache ambazo hata hivyo hazikua za wazi sana kutokana na maumbile makubwa ya walinzi wa Mali ambao waliwanyima nafasi washambuliaji Yohana Mkomola na Asad Juma.

Pamoja na walinzi wa Tanzania chini ya Dickson Job na Israel Mwenda wakisaidiwa na walinzi wa pembeni Nickson Kibabage na Kibwana Shomari  pongezi nyingi zinapaswa kuelekezwa kwa mlinda mlango Ramadhan Kabwili ambaye alifanya kazi kubwa ya kuokoa makombora mazito bila wasiwasi wowote.

Serengeti Boys watarejea tena dimbani May 18 kuwakabili Angola ambao wao wapo dimbani sasa hivi wakivaana na Niger.

No comments

Powered by Blogger.