YANGA YAIKIMBIA SIMBA KIAINA KOMBE LA FA, YAKUBALI KUFUNGWA NA MBAO
Mabingwa watetezi wa michuano ya kombe la Shirikisho Tanzania bara maarufu kama kombe la FA Yanga wameangukia pua baada ya kufungwa bao 1-0 na Mbao FC ya jijini Mwanza.
Mchezo huo wa nusu fainali ya pili ulichezwa jioni ya leo kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa na kushuhudiwa na maelfu ya mashabiki wa jiji la Mwanza na Viunga vyake.
Dakika 15 za awali zilitawaliwa na Yanga huku Mbao wakijaribu kuwasoma na kuweza kubadilika dakika 15 zilizofata na kuganikiwa kupata bao la kuongoza dakika ya 27 mlinzi wa Yanga Andrew Vicente akijifunga baada ya shambulizi kali la Mbao wakitumia winga.
Licha ya Yanga kurejea kipindi cha pili kwa nguvu mpya wakijaribu kutafuta bao la kusawazisha lakini walishindwa kabisa kuipita ngome ya Mbao na kufanya mchezo huo kumalizika kwa ushindi huo wa bao 1-0 kwa Mbao.
Matokeo hayo yanaifanya Mbao sasa kufanikiwa kutinga Fainali kwa mara ya kwanza katika msimu wao wa kwanza tangu walipopanda kwenye ligi kuu na watacheza fainali dhidi ya Simba mwishoni mwa mwezi wa tano lakini pia lile wazo la kuziona Simba na Yanga zikikutana katika fainali limefutika baada ya mechi hii.
No comments