KAMATI YA KATIBA HADHI NA SHERIA KUKAA KESHO
Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), inatarajiwa kukutana Jumanne kwa lengo la kupitia uamuzi uliofanywa na Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji Ligi Tanzania maarufu kwa jina la Kamati ya Saa 72.
Kwa mujibu wa Katiba ya TFF, Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF, ina mamlaka ya kutafsiri sheria na kanuni za mpira wa miguu nchini kama ilivyoainishwa kwenye katiba na sehemu ya utangulizi ya kanuni za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Kamati hiyo inakutana kutokana na ombi la timu ya Kagera Sugar ambayo imeomba kupitiwa upya uamuzi uliofanywa na Kamati ya Saa 72 ambayo kwa mujibu wa kanuni, ilitoa matokeo mapya ya mchezo kati ya timu hiyo na Simba uliofanyika Aprili 2, mwaka huu huko Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera.
Katika mchezo huo, Kagera Sugar ilishinda mabao 2-1, lakini Simba ilikata rufaa ikidai kuwa Kagera Sugar ilivunja kanuni ya 37 (4) ya Ligi Kuu ya Vodacom kwa kumchezesha mchezaji Fakhi Mohammed ambaye alidaiwa na Simba kuwa alikuwa na kadi tatu za njano katika mechi tofauti za Liku Kuu ya Vodacom. Hivyo, ikaadhibiwa kwa mujibu wa kanuni ya 37 (37) ambayo ilitoa pointi tatu na magoli matatu kwa Simba.
No comments