MPINZANI WA YANGA CAF KUJULIKANA KESHO
Mpinzani wa Yanga katika mchujo wa kuwania hatua ya
makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika anatarajiwa kujulikana kesho katika droo
itakayopangwa mchana mjini Cairo, Misri yalipo makao makuu ya Shirikisho la
Soka Afrika (CAF).
Droo hiyo itahusisha timu zilizovuka hatua ya 32
Bora ya Kombe la Shirikisho dhidi ya zilizotolewa kwenye hatua hiyo ya Ligi ya
Mabingwa Afrika.
Timu zilizotolewa Ligi ya Mabingwa zitamenyana na
zilizosonga mbele Kombe la Shirikisho katika mechi za nyumbani na ugenini
kuwania nafasi ya kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa
kwa ngazi ya klabu barani.
Mechi za kwanza zinatarajiwa kucheza wikiendi ya
Aprili 7 hadi 9 na marudiano yanatarajiwa kuwa wikiendi ya Aprili 14 hadi 16,
mwaka huu.
Timu zilizovuka hatua ya 32 Bora Kombe la Shirikisho
ni MC Alger, JS Kabylie za Algeria, Recreativo do Libolo ya Angola, ASEC
Mimosas ya Ivory Coast, El Masry, Smouha ya Misri, MAS Fes, Ittihad Tangier za
Morocco, Rayon Sports ya Rwanda, Hilal El Obeid ya Sudan, Mbabane Swallows ya
Swaziland, Platinum Stars, Supersport United za Afrika Kusini, Club Africain,
CS Sfaxien za Tunisia na Zesco United ya Zambia.
Zilizotolewa Ligi ya Mabingwa ni RC Kadiogo ya
Burkina Faso, AC Leopards ya Kongo, AS Tanda ya Ivory Coast, TP Mazembe ya DRC,
Gambia Ports Authority ya Gambia, Horoya ya Guinea, CNaPS ya Madagascar, AS
Port Louis ya Mauritius, FUS Rabat, Wydad Athletic Club ya Morocco, Ferroviario
Beira ya Msumbiji, Rivers United, Rangers ya Nigeria, Bidvest ya Afrika Kusini,
Yanga SC ya Tanzania ya KCCA ya Uganda.
Yanga SC imengukia Kombe la Shirikisho Afrika baada
ya kutolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa baada ya sare ya 0-0 na
wenyeji, Zanacio Jumamosi Uwanja wa Taifa wa Mashujaa, Lusaka nchini Zambia.
Matokeo hayo yanamaanisha Yanga inatolewa kwa mabao
ya ugenini, baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 kwenye mchezo wa kwanza wiki
iliyopita Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

No comments