SAFARI HII SIKUKUU ZITAPAMBWA NA LIGI KUU YA VODACOM, RATIBA NZIMA IPO HAPA.

Mechi 14 za Ligi Kuu ya Vodacom zinatarajiwa kupigwa wakati huu wa msimu wa kufunga mwaka 2016 kisha mbili zitaufungua mwaka mpya 2017.



Azam TV, wadhamini wenza wa ligi hiyo, wamewathibitishia mashabiki wa soka nchini kupata burudani kwa michezo yote kulingana na ratiba.

Michezo 15 ya kipindi cha sikukuu za kufunga na kufungua mwaka inatarajiwa kuanza saa 10.00 jioni isipokuwa ule wa Mbao FC na Mwadui uliopangwa kuanza saa 8.00 mchana kama itakavyojieleza hapo chini kwenye mtiririko wa ratiba.

Mchezo wa kesho Ijumaa Desemba 23, utazikutanisha timu za African Lyon na Young Africans kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, sheria 17 zikisimamiwa na Mwamuzi, Ludovic Charles kutoka mkoani Tabora.

Jumamosi Desemba 24, 2016 utaona mechi sita. Mbeya City wataikaribisha Toto Africans kwenye dimba la Sokoine jijiji Mbeya. Kipyenga kitajazwa upepo na mwamuzi Shakaile ole Shangalai wa Pwani.

Huko Kaitaba kwenye nyasi bandia Kagera Sugar watawaalika Stand United katika. Mwamuzi akiwa ni Jacob Adongo wa Mara.

Ndanda watabaki nyumbani Nangwanda Sijaona, Mtwara wakiwa na mning'inio baada ya kufungwa na Simba juma lililopita, sasa watawakaribisha Mtibwa Sugar na mwamuzi atakuwa Andrew Shamba wa Pwani.

Vinara wa ligi Simba na JKT Ruvu watatoana jasho Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam wakisimamiwa na mwamuzi Hans Mabena wa Tanga.

Baada ya kulala Mbeya mbele ya Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine, Majimaji ya Songea itakuwa mwenyeji wa Azam FC ya Dar es Salaam ambayo juma lililopita iliambulia sare tasa kutoka kwa African Lyon. Majimaji na Azam zinakutana katika Uwanja wa Majimaji mjini Songea.

Mwadui ambayo ilianza vibaya duru la pili kwa kupoteza mchezo uliopita, itakuwa mwenyeji wa Mbao FC ya Mwanza kwenye Uwanja wa Mwadui Complex mkoani Shinyanga
Mchezo utakaoanza saa 8.00 mchana ili kutoa fursa kwa mdhamini Azam kuonesha mchezo huo mubashara.

Sikukuu ya Krismas, yaani Desemba 25, 2016 hakutakuwa na mchezo ila siku inayofuata Desemba 26, Ruvu Shooting itakuwa mwenyeji wa Tanzania Prisons ya Mbeya kwenye Uwanja wa Mabatini, ulioko Mlandizi mkoani Pwani.

Desemba 28, kutakuwa na mechi mbili ambapo Young Africans ya Dar es Salaam itakuwa mwenyeji wa Ndanda ya Mtwara kwenye Uwanja wa Uhuru jijini huku Majimaji ya Songea ikiwa mgeni wa Mtibwa Sugar ya Morogoro kwenye Uwanja wa Manungu ulioko Mvomero.

Desemba 29, Ruvu Shooting ya Pwani inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Simba ya Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam katika mchezo ambao mwamuzi atakuwa Alex Mahagi wa Mwanza.

Siku hiyo hiyo Azam ya Dar es Salaam itatulia nyumbani Uwanja wa Azam huko Chamazi ikicheza na Tanzania Prisons ya Mbeya.

Saa kadhaa kabla ya kuingia mwaka 2017, yaani Desemba 31, mwaka huu kutakuwa na mchezo ambapo Mwadui ya Shinyanga itacheza na Kagera Sugar ya Kagera kwenye Uwanja wa Mwadui mkoani Shinyanga.

Kadhalika siku ya funga mwaka, Mbeya City inatarajiwa kucheza na Mbao FC kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya kisha
Januari mosi sikukuu ya mwaka mpya kutakuwa na michezo miwili tu ya kukaribisha Mwaka Mpya ambapo Toto African ya Mwanza itacheza na Stand United ya Shinyanga kwenye uwanjabwa Kambarage huku African Lyon ya Dar es Salaam ikiwa mwenyeji wa JKT Ruvu Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Mara baada ya michezo hiyo, Ligi Kuu ya Vodacom itasimama kwa wiki mbili kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi inayotarajiwa kuanza Januari mosi, mwaka huu

No comments

Powered by Blogger.