WIKIENDI YA UPINZANI WA JADI KATIKA LIGI 5 MAARUFU BARANI ULAYA. JE UTAWEKA MIKEKA MINGAPI?

Na Frank LeLo.
Burudani ya soka inarudi kwa kishindo wikiendi hii baada ya kumalizika kwa mechi za kimataifa. Hakutakua na mechi za kimataifa tena mpaka mwezi machi 2017. Kwa iyo kuanzia kesho jumamosi mpaka mwezi machi tutaziangalia klabu zetu pendwa kila wiki huku tukifurahia kwa tutakaoshinda na kusikitika kwa tutakaofungwa.
Wikiendi hii itakua ya kusisimua sana. Kuna mechi kubwa nyingi katika ligi nne au tano barani ulaya. Manchester united itawakaribisha Arsenal. Borrusia Dortmund itawakaribisha Bayern Munich, AC Milan itavaana na Inter Milan, Athletico Madrid itawakaribisha Real Madrid na kule Uturuki Fernebance itawakaribisha Galatasary.
Wale ndugu zangu wanaopenda kubashiri matokeo kwa kamari au kwa kiingereza "kubet" au maarufu kama mikeka, hakika hii ni wikiendi ambayo ukichezesha karata zako vizuri, unaweza kulala maskini ukaamka tajiri.
Mimi sitakushauri uweke mikeka yako kwa timu ipi. Katika makala hii tutaziangalia timu hizi kwa undani, kuangalia mwenendo wa timu zote kwa wiki za hivi karibuni na nitakuachia wewe utoe maamuzi na utabiri mwenyewe.
MANCHESTER UNITED VS ARSENAL (UWANJA WA OLD TRAFFORD)
Je ni muda sahihi wa Wenger kumfunga Mourinho?
Tunaweza kusema mdomoni kua mechi ya Manchester United vs Arsenal sio pambano kati ya Jose Mourinho na Arsene Wenger. Lakini tutakua tunajidanganya, jibu ni ndio! Hili pambano linawahusu
wao binafsi pia.
Kila mtu anajua makocha hawa hawapendani kabisa na hata wakisalimiana kesho, watasalimiana kutimiza wajibu tu lakini mioyoni mwao wanatamani hata wasikutane waangaliane uso kwa uso. Kwa wote hawa, kufungwa sio jambo litakalokubalika jumamosi hii.
Lakini kwa suala la rekodi, Mourinho anaweza kujivunia na kumtambia Arsene Wenger. Katika mechi 13 za kiushindani Mourinho ameshinda mechi 7 huku akitoa sare 6. Kwa maana hiyo hajawahi kufungwa hata mechi moja na Arsene Wenger. Mechi moja aliyopoteza dhidi ya Wenger ni ile ya kombe la ngao ya hisani, akifungwa 1-0 na Arsenal akiwa kocha wa Chelsea. Sio jambo la kujivunia kabisa kwa Arsene Wenger na mashabiki wa Arsenal.
Arsene Wenger daima atakua na kumbukumbu mbaya dhidi ya Mourinho. Katika mechi yake ya 1000 kama kocha mkuu wa Arsenal, alifungwa 6-0 na Chelsea iliyokua inafundishwa na Mourinho mwaka 2014 kwenye mechi ya ligi kuu ya Uingereza. Hii ni moja ya kumbukumbu mbaya kabisa ya Arsene Wenger kwenye maisha yake ya Soka. Lakini bado ana nafasi ya kulipa kisasi. Je Jumamosi ndo nafasi yenyewe?
Manchester united ilianza ligi vizuri lakini hapa katikati mipango imeharibika na haijapata matokeo mazuri hali ambayo imetengeneza wasiwasi kwa mashabiki wa Manchester United. Pia wachezaji muhimu wataikosa mechi hii kwa sababu za majeruhi na kufungiwa kama adhabu. Zlatan Ibrahimovic, Chris Smalling, Eric Baily, Antonio Valencia na Marounne Fellaini wote wanategemewa kuikosa mechi hii.
Kwa upande wa Arsenal, Mambo si mabaya sana. Imefungwa mechi moja tu msimu huu na katika mechi 12 zilizopita wameshinda mechi 10. Wachezaji muhimu kama Mesut Ozil, Theo Walcot, Granit Xhaka, Shkrodan Mustafi, Alexi Iwobi na Alexis Sanches wapo kwenye morali nzuri na wanacheza vizuri. Je ni muda muafaka wa Arsene Wenger kufuta uteja kwa Mourinho? Jibu tutalipata Jumamosi mchana.
ATHLETICO MADRID VS REAL MADRID. DIEGO SIMEONE ANATAFUTA KULIPA KISASI CHA FAINALI UEFA MWEZI MAY 2016.
Mechi kubwa katika ligi ya Hispania hadi sasa kwa msimu huu lakini pia marudio ya mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa msimu uliopita. Ni mechi ya upinzani wa jadi kwa timu zinazotoka jiji maarufu la Madrid nchini Hispania. Kama ilivyo hapa kwetu "Dar es Salaam derby" kati ya Simba na Yanga.
Kwa miaka ya karibuni Athletico Madrid wamekua wakiiletea Real Madrid usumbufu na hawajafungwa na Real Madrid katika mechi 13 zilizopita ndani ya dakika 90 za kawaida za mchezo. Real madrid imeifunga Athletico Madrid mara 2 tu zote zikiwa mechi za fainali ya mabingwa wa ulaya na mechi zote hizo zikiamuliwa kwa matuta na kwa dakika za nyongeza baada ya zile dakika 90 za kawaida.
Msimu huu umekua si wa kuridhisha sana kwa Athletico Madrid. Falsafa yao imebadilikia kidogo kutoka kucheza staili ya kukaba na kushambulia kwa kushtukiza zaidi kuhamia kwenye falsafa ya kushambulia zaidi kwa muda mrefu ili wachezaji nyota kama Kevin Grameiro, Antonie Griezman na Yannick Carrasco waweze kung'aa zaidi.
Lakini kutumia aina hii ya mchezo kuna gharama zake moja ikiwa unakua na hatari ya kuruhusu magoli kwa sababu timu inadhamiria kushambulia zaidi kuliko kukaba. Na ndivyo ambavyo imewatokea Athletico Madrid msimu huu, katika mechi 3 zilizopita za ligi wamepoteza michezo mitatu na hivyo kuachwa pointi kadhaa na viongozi wa ligi Real Madrid. Kupata matokeo dhidi ya vijana wa Real Madrid itakua mtihani na itawalazimu kukaza beki yao ili kutimiza lengo.
Kwa upande wa Real Madrid bado na wao hawajakaa mkao wa kula. Matokeo yamekua sio mazuri moja kwa moja, wakipata sare nyingi katika mechi za hivi karibuni. Gareth Bale ndie mchezaji ambae amekua akiifungia timu hii magoli muhimu kwa siku za karibuni.
Mchezaji wao bora Christiano Ronaldo bado hajakaa kwenye kiwango chake tulichokizoea na wachezaji muhimu kama Sergio Ramos, Casemiro, Luka Modric na Karim Benzema wakitoka majeruhi ya muda mrefu. Pamoja na hayo Real madrid bado haijafungwa mechi yoyote katika mashindano yoyote msimu huu.
BORUSSIA DORTMUND VS BAYERN MUNICH
Mechi hii inajulikana kwa jina maarufu la Kijerumani liitwalo "De Klassiker". Bayern Munich imekua ikitawala ligi ya Ujerumani maarufu kama Bundesliga. Lakini Borussia Dortmund katika miaka ya hivi karibuni imekua ikileta upinzani mkali. Tangu Jurgen Klopp (kocha wa Liverpool hivi sasa) aanze kuifundisha Dortmund mwaka 2008 ameifanya kua timu ya ushindani sana ikichukua ubingwa wa Ujerumani mwaka 2011 na 2012 na kucheza fainali ya mabingwa ulaya mwaka 2013.
Katika mechi 11 zilizopita kati Bayern na Dortmund, Bayern ameshinda mechi 4 na kutoa sare 3, zilizobaki Dortmund wameibuka kidedea. Hii inaonesha ni kwa kiasi gani ushindani baina yao ulivyo wa karibu. Timu zote mbili zina makocha wapya. Tomas Tuchel alieanza kuifundisha Dortmund msimu uliopita na Muitaliano Carlo Anceloti aliepokea mikoba ya Pep Guardiola pale Bayern Munich msimu huu.
Bayern hawajafungwa mechi yoyote msimu huu kwenye ligi ya bundesliga na wanaongoza ligi kwa tofauti ya magoli tu lakini wamekua wakitoa sare hivi karibuni (sare 3 katika mechi 10). Dortmund ni moja ya timu zinazovutia kuangalia msimu huu wakitandaza soka safi ya kushambulia na wachezaji wao wengi ni vijana wa umri wa kati. Lakini matokeo yamekua si ya kuridhisha moja kwa moja. Moja ya vitu vitakavyowatia morali Dortmund kwenye mechi hii ni kurudi kikosini kwa mchezaji muhimu mshambuliaji Marco Reus aliekua majeruhi tangu mwezi May mwaka huu.
Marco Reus, Pierre Emerick Aubameyang na Mario Gotze wanaweza kutengeneza moja ya safu ya ushambuliaji ambayo inaweza kuipenyeza ngome yoyote ngumu kwa sababu ya vipaji walivyonavyo wachezaji hawa. Ni mechi nzuri kwa mashabiki wa soka na ni ngumu kutabiri nani atashinda.
AC MILAN VS INTER MILAN
Hii itakua ni mechi ya 165 kati ya watani hawa jadi wanaotoka jiji moja maarufu kule nchini Italia, jiji la Milan. Mechi hii inajulikana kwa jina maarufu kama "Derby della Madonnina" ni moja ya mechi yenye utajiri wa kihistoria na moja ya mechi ambazo kwa miaka mingi imekua na umuhimu kwenye ramani ya soka na hata ulimwenguni kote. Mambo yamekua tofauti kwa miaka ya karibuni
kwani timu hizi zilizojizolea umaarufu mkubwa kwa sababu ya mafanikio yao barani ulaya zimekua zikisua sua sana n Juventus inatawala ligi hiyo kwa miaka 6 sasa. Mwezi ujao tarehe 13, Kikundi cha wawekezaji wa kutoka China itamalizia utaratibu mzima wa kununua hisa za AC Milan na na itaashiria mwisho wa utawala wa Silvio Berlusconi / Adriano Galliani ambao umechangia mataji matano ya ubingwa wa Ulaya (UEFA Champions league) kati ya 7 ambayo AC Milan imeyanyakua.
Kwa msimu huu Inter Milan imeendela kufanya vibaya. Matokeo yamekua mabovu kiasi cha kupelekea kufukuzwa kwa kocha Frank De Boer aliedumu kibaruani kwa miezi mitatu tu. Inter ina wachezaji wazuri na pia imefanya usajili mkubwa lakini bado matokeo yamekua si ya kufurahisha. Stefano Pioli ndio kocha Inter Milan hivi sasa na ameteuliwa wiki 2 zilizopita. Amefanya kazi na kikosi hicho kwa wiki mbili tu na kibarua chake cha kwanza ni kupambana na watani wa jadi AC Milan.
AC Milan imeanza vizuri msimu huu ukilinganisha na misimu michache iliyopita. Vincenzo Montella aliekabidhiwa kibarua cha kuionoa timu iyo amewekeza imani yake kwa kikosi cha vijana zaidi na amepata matokeo mazuri hadi hivi sasa.
Timu zote hizi kutoka jiji la Milan zinapambana ili kurudia hadhi yao ya zamani na kurudi kushiriki michuano ya ligi ya mabingwa Ulaya kama ilivyokua desturi. Kitu cha kufurahisha timu zote hizi mbili zimeshaifunga Juventus msimu huu, hii inaonesha ni kwa kiasi gani mechi hii itakua kali na ya kusisimua hii.
No comments