MALINZI AMLILIA MZEE SAID MOHAMED, ASEMA ALIKUA HAZINA.
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za
kifo cha Mwenyekiti wa Azam FC na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu, Sheikh
Said Mohammed aliyefariki dunia leo Novemba 7, 2016 katika Hospitali ya Aga
Khan, Dar es Salaam.
Taarifa za kufariki dunia kwa Mzee
Said Mohammed ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi zimethibitishwa
na Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba aliyesema kwamba alifariki dunia
katika wodi ya Wagonjwa mahututi (ICU) hospitalini hapo baada ya kuzidiwa
ghafla nyumbani kwake.
Kutokana na kifo hicho, Rais wa TFF
Malinzi ametuma salamu za rambirambi kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Yahya
Mohammed, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura, Uongozi wa Klabu ya
Azam, familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki. Amewataka kuwa watulivu
wakati huu mgumu wa kumpoteza Mzee Said Mohammed.
Katika salamu zake, Malinzi
amemwelezea marehemu Said Mohammed kuwa alikuwa hazina katika mpira wa miguu
nchini kutokana na uwezo wake mkubwa wa kutoa mchango ya mawazo na miongozo
katika Kamati ya Utendaji ya TFF.
Aliongoza Klabu ya Azam kwa
mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kubeba ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara na Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup)
kwa mara ya kwanza tangu klabu hiyo ianzishwe.
“Ndani ya Kamati ya Utendaji ya TFF,
Mzee Mohammed ndiye aliyekuwa na umri mkubwa ukilinganisha na wajumbe wengine,
lakini alikuwa hakosi vikao muhimu. Mchango wake wa mawazo ulikuwa nguzo kwetu.
Nimepokea taarifa hizi za kifo chake kwa masikitiko makubwa,” amesema Rais
Malinzi leo mara baada ya kupokea taarifa za kifo hicho.
Taratibu za mazishi zinafanywa
nyumbani kwa marehemu. Sheikh Said Mohammed atazikwa leo alasiri katika
makaburi ya Kisutu baada ya mwili wake kuswaliwa msikiti wa Maamur ulioko
Upanga, jijini Dar es Salaam.
Inna lillah wainn ilayh
Rajiuun.
No comments