KUTANA NA KOCHA MWENYE UMRI MDOGO ZAIDI ANAYESUMBUA WAKONGWE BUNDESLIGA
Julian Nagelsmann! Ni jina geni masikioni mwa mashabiki wengi wa soka duniani, lakini si kwa wale wa ligi kuu ya Ujerumani, Bundesliga! Akiwa na umri wa miaka 29 tu, huyu ni kocha mwenye umri mdogo zaidi ndani ya ligi kubwa za barani Ulaya.
WASIFU WAKE.
Amezaliwa July 23, 1987 huko Landberg am Lech, Munich, Ujerumani. Akiwa na miaka 15 tu alianza kucheza soka akiwa kama beki ndani ya klabu ya Augsburg, na baadae kuhamia klabu ya 1860 Munich. Hata hivyo hakufanikiwa kucheza mchezo wowote rasmi wa timu za wakubwa, na kwa bahati mbaya zaidi akaacha kucheza mpira akiwa na miaka 20 tu baada ya majeraha ya goti ya mara kwa mara.
SAFARI YA UKOCHA.
Baada ya kuachana na soka, aliamua kwenda kusomea Sayansi ya Michezo (Sports Science), na baadaye kujiingiza kwenye ukocha. Alianza ukocha kwenye timu za vijana za klabu zake za zamani za Augusburg na 1860 Munich, na mwaka 2010 akiwa na miaka 23 tu alikabidhiwa kukinoa kikosi cha under-17 cha klabu yake ya sasa ya TSG Hoffenhaim.
Miaka 3 mbele akiwa na miaka 26, aliaminiwa na kupewa kikosi cha under-19 ambacho alikiongoza kupata ubingwa wa kitaifa Ujerumani msimu wa 2013/2014, na baadae kufika fainali tena kwa msimu wa 2014/2015.
Pamoja na klabu kubwa kama Bayern Munich kuvutiwa naye na kutaka kumpa kazi ya ukocha kwenye timu yao ya under-23, Nagelsmann aliendelea kubaki klabuni Hoffenheim baada ya uongozi kuwa na mpango wa kumpa rasmi ukocha mkuu mwishoni mwa msimu wa 2015/2016.
Mwezi February 2016, kocha mkuu wa Hoffenheim Huub Stevens alilazimika kuachia ngazi kwa matatizo ya kiafya, na ndipo Nagelsmann alipopewa mikoba ya kuiongoza timu mpaka mwisho wa msimu.
Kazi yake kubwa ya kwanza ikawa ni kujaribu kuibakiza timu kwenye ligi kuu, kwani Hoffenheim ilikuwa na hali mbaya kwa wakati huo. Timu ilikuwa kwenye vita ya kutoshuka daraja, ikiwa imeshinda michezo 2 pekee, huku ikiwa nafasi ya 2 toka mkiani, na pointi 5 pungufu toka kwenye nafasi za mtoano wa kubaki ligi kuu.
Tofauti na matarajio ya wengi, kamali ya uongozi wa Hoffenheim kumpa timu kocha huyu kijana ikalipa. Nagelsmann akashinda michezo 7, sare 2 na kufungwa 5 kwenye mechi 14 zilizokuwa zimebaki. Kwa pointi 23 ilizojikusanyia, Hoffenheim ikabaki ligi kuu ikiwa nafasi ya 15.
Msimu huu wa 2016/2017 umekuwa kama mwendelezo tu wa mafanikio ya Nagelsmann na Hoffenheim kiujumla. Mpaka sasa, Hoffenheim iko nafasi ya 3 kwenye Bundesliga, imeshinda mechi 5 na sare 5 na ni moja ya timu 3 pekee ambazo hazijapoteza mchezo wowote (nyingine ni mabingwa Bayern Munich na wageni RB Leipzig walio nafasi za 1 na 2). Wao pamoja na Leipzig wamekuwa ni timu 2 zinazoshangaza zaidi msimu huu kwenye Bundesliga, na wameshinda mechi 4 mfululizo kabla ya kupisha mechi za kimataifa.
FALSAFA YAKE.
Nagelsmann anaamini mafanikio ya timu kwake yeye yanategemea zaidi ubora wa mchezaji kuliko mfumo.
Anasema kwenye ukocha, 30% anategemea mbinu, na 70% anategemea utimamu wa kisaikolojia wa wachezaji wake. Anadai kila mchezaji ana mahitaji yake na namna yake ya kumpa hamasa, kwa hiyo ni muhimu kwake kama kocha kujua nini kinamuweka sawa kisaikolojia mchezaji yupi, kabla hajatarajia wachezaji kucheza vizuri kwenye mfumo fulani anaoutaka!
Akiwa ni msomi wa Sayansi ya Michezo, Nagelsmann ni muumini wa data za kisayansi, na eneo mojawapo analopendelea kuzingatia ni muda ambao wachezaji hutumia uwanjani bila kupata mpira, na hilo analitumia sana kuboresha viwango wachezaji wake na timu kiujumla.
Huyo ndiye Julian Nagelsmann, bwana mdogo anayetikisa Bundesliga, na ambaye naamini ndani ya miaka kadhaa atakuwa gumzo duniani kote!
Maswali ya kujiuliza ni je, ataendelea na mwendo huu mpaka mwisho? Hoffenheim wataweza kumshikilia kwa muda mrefu? Umri na uzoefu ni muhimu kwenye kuongoza timu hasa kwenye kizazi hiki chenye maendeleo kisayansi na teknolojia?
....Imeandaliwa na Jerry Billinje (Member:Wapenda Soka Tanzania)
No comments