YANGA YAENDELEA KUGAWA DOZI NA SAFARI HII ILIKUA ZAMU YA MBAO

Yanga hawakutaka mchezo kabisa mbele ya wabishi wa Mbao FC kutoka Jijini Mwanza baada ya kuwashindilia mabao 3-0 katika uwanja wa uhuru jijini Dar es Salaam.



Wakichagizwa na urejeo wa kocha wao Hans Van Pluijm, Yanga waliutawala mchezo huo kwa kipindi kirefu ingawa walinzi wenye nidhamu ya hali ya juu wa Mbao walionekana kuhimili vishindo vya wanajangwani hao.

Mpaka mapumziko kila timu ilikua salama kwa maana ya bila kuruhusu nyavu kutikisika lakini mambo yalikua tofauti katika kipindi cha pili.

Mpira wa adhabu uliopigwa na Haruna Niyonzima katika dakika ya 49 ulitua katika kichwa cha Vicent Bossou, ukagonga mlingoti wa lango la mbao kabla ya Bossou kuusukumiza wavuni kuiandikia Yanga bao la ufunguzi.

Bao hilo lilizidisha zaidi kasi ya Yanga ambao walianza kulisakama lango la Mbao kama nyuki lakini vijana wa Mbao hawakuchanganya sana na mashambulizi hayo.

Katika dakika ya 55, Mpira uliorushwa kwa nguvu na Mbuyu Twite ulimteleza golikipa wa Mbao Emmanuel Mseja na kutinga moja kwa moja kimiani kuwaandikia Yanga bao la pili.

Yanga waliandika bao la tatu mnamo dakika ya 75 likifungwa na Amisi Tambwe baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Haruna Niyonzima.

Hadi kipyenga cha mwamuzi Ludovic Charles kinapulizwa, Yanga wakaibuka na ushindi wa mabao 3-0.

Ushindi huo umewawezesha Yanga kufikisha point 27 wakiendelea kuwakimbiza kwa mbali vinara Simba wenye pointi 32.

No comments

Powered by Blogger.