WANA - YANGA TUUELEWE MKAKATI WA MANJI ILI KLABU YETU INUFAIKE.

KLABU ya Yanga ipo katika mchakato wa mabadiliko kiungozi na kiumiliki utakaodumu kwa miaka 10 ijayo,Mwenyekiti  Yusuf Manji aliomba ridhaa ya kuikodisha Yanga kwa muda huo ambapo gharama za klabu kuhusiana na mishahara, Usajili, Safari na gharama nyingine zitakuwa upande wake pia klabu itapata mgao wa 25% ya faida ambayo mkodishwaji ataipata lakini ikiwa kuna Hasara basi yeye ndie ataibeba yote na si Klabu au Wanachama.Manji alifafanua kuwa uendeshwaji wa Klabu kwa mfumo huo utahusu Timu na Nembo tu wakati Majengo ya Klabu yanabakia kwa Wanachama.

Katika mkutano mkuu uliofanyika Agost 6 Manji alitoa pendekezo hilo ambalo liliungwa mkono na wanachama wote waliohudhuria mkutano huo.Mjumbe wa bodi ya wadhamini Francis Mponjoli Kifukwe aliahidi wao kama bodi watayafanyia kazi mapendekezo hayo kisheria na kitaratibu kwa maslahi ya klabu ya Yanga SC. Takribani miezi miwili imepita ndipo mkataba wa ukodishwaji ukawekwa wazi, katika mkataba huo ambao kuna vipengele vimeongezwa ili kumbana mkodishwaji na kuhakikisha klabu inanufaika kiuchumi na kimaendeleo uwanjani (rejea mkataba huo). Kampuni ya Yanga Yetu inatajwa kama mkodishwaji.

Sasa Kumekuwa na malumbano, hoja kila upande ukijaribu kuushambulia upande mwingine!mbaya zaidi hoja nyingi zimeonekana sio kujenga bali ni kuukatisha tamaa upande mwingine ama kuvuruga kabisa mpango huo wa ukodishwaji. Baraza la michezo kupitia kwa katibu mkuu wake Mohamed Kiganja walitoa kauli yao "Ili Yanga iweze kubadili jina na kuitwa Yanga Yetu ni lazima ipite kwa msajili. Wao hawajaenda kwa msajili wanaanza kutangaza jina jipya. Huko ni kupinga katiba,".Kwa kauli hii unagundua kabisa jinsi gani vyama vyetu vya michezo vimebeba watu wasio na ufanisi katika taalum ya uongozi wa mpira, watu ambao ni wakurupukaji na wasio na nia thabiti kuupeleka mpira wetu mbele. Kiganja alipinga hadharani kuwa haiwezekani Yanga SC wabadili jina na kuitwa Yanga Yetu ilhali katika mkataba huo Yanga Yetu imetajwa kama kampuni mkodishwaji, usishangae hao ndio viongozi wetu tuliowapa dhamana. Baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa mstari wa mbele kuupotosha umma wa wanamichezo, inasikitisha kuona mkataba ukifafanuliwa kwa minajiri ya kuonekana ni mkataba wa kinyonyaji na hasara kwa Yanga SC. Ni Manji huyu huyu aliyeuzika mgogoro wa Yanga asili dhidi ya Yanga kampuni, aliyetoa hela yake ya mfukoni kufidia gharama za uendeshaji wa klabu, aliyeipa taswira mpya Yanga ionekane klabu bora yenye mishahara mizuri na mazingira bora kiutendaji leo anashutumiwa kuinyonya Yanga SC!ni miaka 10 sasa toka Manji awe mfadhili, mdhamini na sasa mwenyekiti wa Yanga lakini mazuri yote aliyoyafanya kwa miaka 10 inafunikwa na watu wachache wanao ona mfumo wa ukodishwaji hautawanufaisha.

Nilipata kumuuliza swali mmoja wa kiongozi wa TFF "Kwanini Azam iliyoanzishwa mwaka 2007/2008 ina maendeleo kuvizidi vilabu vya Simba na Yanga vilivyoanzishwa 1936 na 1935?" Jibu lake lilikuwa rahisi sana kuwa mfumo wa uendeshwaji, akaenda mbali zaidi kuwa vilabu vya Yanga na Simba vimeasisiwa katika mfumo huu na kamwe wao hawatabariki mabadiliko mengine kiungozi/kiumiliki kwa vilabu hivi viwili, juhudi zote zinazofanywa na wanachama na viongozi wa vilabu hivi kujikwamua katika aibu kumbe ni bure. Leo viongozi, wanachama, mashabiki wa Simba wanafurahi kuona juhudi za Manji zikielekea kukwama pasipo kujua wapo katika mkondo ule ule au ndo kudhihirisha ule msemo "KUNI YA AKIBA HUICHEKA INAYOUNGUA"?

Ni vigumu kufikia malengo kama bado klabu ipo mikononi mwa mfumo zilipendwa, Mfumo wenye kuwapa sauti baraza la wazee ambalo kikatiba halitambuliki!mfumo ambao unatoa nafasi kwa wajuaji wengi wenye maono tofauti kuwa na maamuzi ya kiuongozi_____ unapofikiria kuifanyia Yanga jambo la heri mwingine anawaza heri gani Yanga itanifanyia?? Kupitia kampuni ya Yanga Yetu, Manji anawekeza katika umiliki wa nembo yaani "brand management contract" na mfumo wa uongozi yaani "football team management contract"
“Umeona wapi nembo ya Quality Group ikichezewa na mtu yeyote? Hivyo hata hili la nembo ya Yanga pia lazima iheshimiwe si watu wanapata faida wakati Yanga ibaki kuwa masikini.
“Kwa kutumia nembo ya Yanga, tutazalisha bidhaa mbalimbali za Yanga, zitaingia sokoni zitauzika na Yanga itaingiza fedha na si watu wachache kuingiza fedha halafu klabu haipati chochote,”alisema Manji.

Hebu tujiulize toka mwaka 1935 nembo ya Yanga imeingizia klabu pato lolote?Je mfumo huu wa umiliki na uongozi una tija yoyote kwa soka la sasa?kwa mfumo huu wa tangu zama za ASP na TANU tusitegemee kupiga hatua,soka la sasa linahitaji uwekezaji, soka la sasa linahitaji matajiri kiungozi, soka la sasa linahitaji watu wachache wenye uweledi waweze kufanya maamuzi ya mustakabali wa klabu sio hadi Mzee Akilimali naye awe na sauti. Hatuoni katika nchi za wenzetu zilizoendelea katika mchezo wa soka watu kama Manji ndio wanahitajika au ndo tuamini "DUNIA YA MUNGU VITU VYA MZUNGU"___Shime wana Yanga tuungane kwa sauti na kauli moja kwa manufaa ya klabu yetu tambueni tupo katika vita, isiwe vita ya Manji dhidi ya wanaompinga bali iwe vita ya wanaompinga Manji dhidi ya Yanga pia tukumbuke kulipia kadi za uanachama.

“Sina fedha za kuinunua Yanga ndio maana sijataja kiasi chochote kile kwa sababu najua thamani yake ni kubwa kuliko mtu yeyote yule, halafu nitoe mfano hivi unaweza kumpa kiasi gani mama yako? Kila mtu atakwambia hakuna fedha itakayomtosha hivyo ni kama Yanga, Yanga ni kubwa sana,” moja ya kauli za Manji.

No comments

Powered by Blogger.