LICHA YA KUTOLEWA,MALINZI AWAAHIDI MAKUBWA VIJANA WA SERENGETI BOYS
Rais wa Shirikisho la Mpira
wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amesema kwamba ataendelea kuwa karibu na
vijana na Timu ya Tanzania ya vijana ‘Serengeti Boys’ licha ya kuondolewa na
Congo kwenye harakati za kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa
vijana zitakazofanyika Madagascar Aprili, mwakani.
Mipango ya TFF kwa sasa
inayoongozwa na Malinzi kwa sasa ni kuiiingiza timu hiyo kwenye program ya timu
ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 20 maarufu kwa jina la Ngorongoro Heroes
baada ya kuguswa na kilio cha vijana hao ambao walishindwa kujizuia kumwaga
machozi mbele ya Malinzi ambaye alifanya kazi kubwa kuwatuliza pamoja na
viongozi wengine.
Serengeti Boys ilipoteza mchezo
dhidi ya Congo Oktoba 2, 2016. Kwa kupoteza mchezo huo dakika ya pili kati ya
nne ya nyongeza baada ya kumalizika kwa dakika 90, kumefanya vijana hao wa
Tanzania kuenguliwa kwenye mashindano ya kuwania kucheza fainali za Kombe la
Mataifa ya Afrika – fainali zitakazofanyika Madagascar.
Dakika moja ndiyo iliyoipoteza
Serengeti Boys kufuzu kwa fainali hizo kwa bao la dakika ya 92 la lililofungwa
na Mountou Edoward.
“Niko nanyi, najua mna group la
WhatsApp, naomba msifute namba yangu. Iwe humo na mambo yenu mengi naomba
mniambie humo, na nitayashughulikia iwe binafsi au kiofisi. Nawahakikishia
sitawaacha,” alisema Malinzi alipowafariji vijana hao ambao wanatarajiwa
kuingia leo saa 3.00 usiku huu kwa ndege ya Shirika la Ndege ya Rwanda.
“Umri wenu bado sana wa kucheza
soka. Program za TFF, CAF na FIFA ziko nyingi pia mnaweza kupata nafasi ya
kucheza Olimpiki na kuna michuano mingi, sitawaacha,” alisema Malinzi na
kusisitiza ana imani na timu hiyo ambayo kwa dakika 90 za mchezo dhidi ya Congo
walipambana kwelikweli kutetea taifa lao pendwa Tanzania.
No comments