RASHFORD, MPIGE KOFI MOURINHO.

Hakuna shaka na kipaji chake, hakuna mwenye wasiwasi na kasi yake na hakuna ambaye anaweza kuuliza uwezo uliokuwa kwenye miguu yake na namna ambayo anaweza kuwa rafiki wa nyavu za timu pinzani hasa kwa umri wake. Ana kasi, nguvu na pia ana uwezo wa kucheza nafasi nyingi kwa wakati mmoja. Mshambuliaji wa kisasa kabisa unayeweza kumpata katika uso wa dunia hii ambayo washambuliaji wamekuwa Tanzanite, yaani ni nadra.


Kwa huyu Mourinho hazitaki mbichi, anaringa wakati anamhitaji na anapata wasiwasi wa kutokumpa muda. Dakika zake chache uwanjani kila anapopata nafasi zimekuwa na tija kubwa kiasi kwamba hakuna jicho la mpenda soka ambalo linaweza kufumbwa kila anapogusa gozi. Tangu mara ya kwanza anamwadhibu Arsene Wenger mpaka mara ya mwisho alipotaka kuleta kiburi cha Mourinho juu ya Pep Guardiola.

Anaweza asiwe amekomaa na kuwa mchezaji wa kutegemewa lakini akili yake na ubunifu unamfanya  kuwa egemeo sahihi la Mourinho kipindi ambacho Wayne Rooney akiwa ameenda likizo ndani ya uwanja. Bahati nzuri ni kuwa uwezo wake wa kucheza eneo lote la mbele kwa ufasaha linambeba kuliko pengine mchezaji nwingine ukiondoa Zlatan Ibrahimovic, hata Martial akili yake haijatulia kama huyu linapokuja suala la kutizama goli.

Lakini kipaji peke yake sio jambo ambalo Mourinho analitazama sana. Anahitaji mchezaji anayejituma na anayeweza kumpa mlinganyo sahihi kwa maana ya muunganiko baina ya wachezaji wote ndani ya timu. Uwepo wa Zlatan ambaye yupo katika kiwango bora, unamaanisha hakuna mchezaji mwenye nafasi katika eneo la mshambuliaji wa mwisho.

Kiwango cha Mata pia hakijawa kibovu katika ligi kuu ya Uingereza tangu msimu uanze, pesa ya Henrikh Mkhitaryan inahitaji kuwepo uwanjani na mchezaji bora wa msimu uliopita Martial anatakiwa kucheza na Lingard akiwa na aina ambayo Mourinho anaihusudu. Hivi ndivyo vilivyokuwa vinamweka Rashford katika wakati mgumu wa namna ipi acheze katika kikosi cha Manchester United.

Muda sahihi ulikuwa ni wa Rashford kuusubiri ufike, nyakati njema zilikuwa jirani na kukosa makali katika panga walizoshika wachezaji wanaocheza nafasi yake  kungehitaji kisu alichokumbatia siku moja. Mechi dhidi ya Manchester City alidhihirisha hilo na hata udenda aliomtoa Sam Allardayce akiwa na timu ya Taifa ya vijana ilionyesha hivyo.

Ni ngumu sana kupata nafasi kwa kijana chini ya Mourinho lakini ukiuteka moyo wake naye hukupa mapenzi ya dhati kuliko kokote kule unapoweza kuyapata. Zlatan kamsifia na kuonyesha kumwamini, Mourinho katikisa kichwa kwa maana ya kuhisi ana mzigo wenye thamani miguuni kwake.

Tofauti yake na Martial huyu ni kuwa pamoja na kuwa anaweza kuwa hana maarifa mengi ukilinganisha na mshambuliaji huyu wa Ufaransa, aina yake ya kuwa na mchezowa moja kwa moja na wa kasi unambeba sana. Bahati nzuri anajua kurejea nyuma na kukaba pia, kitu kinachomfanya kuwa aina kabisa ya silaha zinazoweza kutosha kwenye begi analobeba Mourinho.

Hatokuwa na nafasi ya kudumu kwenye ligi kuu ya Uingereza ambako Mourinho anahitaji ushindani wa kila kukicha katika kikosi chake huku akiwa na wachezaji wengi wa kuchagua lakini kwa mashindano yaliyobaki ni mchezaji ambaye anaweza kumpa Mourinho kitu ambacho wengine wote hawana.

Atakaba, atakimbia, atafunga lakini pia atapiga pasi ambayo itakuacha mdomo wazi. Umri wake wa miaka 18 unampa nafasi ya kuendelea kujifunza zaidi, bahati nzuri pia hakuletwa kwa madafu ya gharama kama Martial hivyo hata benchi hakuwezi kumuumiza kichwa wala kumsumbua.

Saikolojia yake itaendelea kukomazwa na uwepo wa mchezaji aina ya Zlatan na ataendelea kujifunza mengi kwake. Aina hii ya wachezaji huitaji timu ambayo kikosi chake hakimpi presha ya kutumainiwa kupita kiasi. Hii ndio silaha ya kukuza kipaji chochote na huku ndiko akina Messi na Ronaldo walipita na ambako Louis Van Gaal aliamua kumrusha kidato Martial kwa kumpa majukumu yaliyomzidi umri.

Nafasi ya Rashford kufanya makubwa naiona ipo jirani, imeshasogea na imefika. Uamuzi ni juu yake kuitumia. Inaweza isifike ikiwa kamili, lakini hata yakija mafungu ni juu yake kuyatumia ipasavyo. Chini ya Mourinho unahitaji kuwa jasusi kweli.

Akikupa nafasi mpige kofi kali, ili ajutie kwanini siku zilizopita hakukupa nafasi. Uwezo unao, nguvu unayo, nia naamini unayo, na nafasi naiona imefika. Weka kiganja chako tayari, yale utakayoyaonyesha uwanjani yawe kofi kwake na asirudie tena. Ukishindwa naweza kuwa wa kwanza kuanza kukusahau, maana huyu mzee anampenda Ibrahimovic pekee kwa dhati.

Nicasius Nicholaus Agwanda (Coutinho Suso)

Follow Instagram @agwandanic

No comments

Powered by Blogger.