HII HAPA RIPOTI KAMILI YA UWANJA WA YANGA KIGAMBONI

Mabingwa wa Soka Tanzania bara Timu ya Yanga (Young Africans Sports Club) imeweka historia muhimu kwenye soka la Tanzania kwa kuzindua mchakato wa ujenzi wa uwanja wa kisasa kabisa wa mpira wa miguu.




 Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. Mwigulu Nchemba (MB) Amezindua rasmi mchakato huo akiwa na mwenyeji wake, Mama Fatma Karume ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Timu ya Yanga.

Akizungumza katika hafla fupi ya uzinduzi huo, Mama Karume alisema “Uwanja huu utakuwa ni mwendelezo wa historia iliyoanzishwa miaka 80 iliyopita ambapo Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Mzee Abeid Karume alitoa eneo la Kaunda kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja cha mpira wa miguu kwa ajili ya timu ya Yanga.” Uwanja wa Yanga wenye viwango vya kimataifa utajengwa eneo la Gezaulole, Kigamboni sambamba na kituo maalum cha kukuza vipaji vya michezo nchini. Naye Mh. Mwigulu alipongeza hatua hiyo na kuitaja kuwa ni chachu madhubuti ya kukuza soka na kuhakikisha mchezo huo unaiweka Tanzania katika nafasi bora kwenye ramani ya soka duniani .

 Timu ya Yanga inauenzi mchango wa Mzee Abeid Karume aliyeipanda mbegu ya kihistoria ambayo imegusa na kuunganisha maelfu ya watu ndani na nje jamii ambao wana imani, kabila na mitazamo tofauti na kuwa kitu kimoja; wapenzi wa mpira wa miguu yaani mashabiki wa timu ya Yanga. Kukamilisha historia ya urithi huu tumempa Mama Karume heshima ya kushuhudia kupanda mbegu ambayo itaweka historia si hapa nchini tu bali duniani kote.

 Mwakilishi wa International Village Ltd, wamiliki wa eneo hilo, Bwana Konstantinos Vasideiadis pia alisema kuwa wana ndoto ya kuufanya uwanja huo kuwa wa kisasa na wa kimataifa. Mchakato kabambe wa mipango ya ujenzi wa uwanja huo utaanza rasmi mwezi Oktoba 2016.

Imetolewa na Uongozi wa Klabu ya YANGA.
YOUNG AFRICANS SPORTS CLUB (YANGA)

P.O.BOX 15202

DAR ES SALAAM

TANZANIA

 Tel: 022 2180011

No comments

Powered by Blogger.