GAVANA WA JIMBO LA AKWA IBOM NIGERIA AWAZAWADIA STARS MAMILIONI KWA KUONYESHA SOKA SAFI
Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), limetuma salamu za shukrani kwa Gavana wa Jimbo la Akwa Ibom,
Gabriel Emmanuel kwa zawadi ya dola 10,000 za Marekani
(sawa na Sh milioni 21.5) kwa timu ya Mpira wa Miguu ya Tanzania ‘Taifa Stars’
baada ya kuonesha mchezo mzuri na wa upinzani dhidi ya wenyeji Super Eagles ya
Nigeria uliofanyika Uwanja wa Kimataifa wa Godswill Akpabo, mjini Uyo.
Taifa Stars ilicheza mechi hiyo
Jumamosi Septemba 3, 2016 katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi kuwania
nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2017). Katika
mchezo huo ambao mashabiki waliingia bure, Taifa Stars ilifungwa bao 1-0 mara
baada ya kuibana Super Eagles hivyo kumsukuma Gavana huyo kuandaa hafla ya
chakula cha jioni ambako mbali ya kuizawadia Stars, pia aliizawadia Super
Eagles dola 35,000 za Marekani.
Taifa Stars ilitua Dar es Salaam
usiku wa kuamkiia leo Septemba 5, 2016 ambako baadhi ya wachezaji
walipelekwa Hoteli ya Urban Rose, iliyoko katikati ya Jiji la Dar es
Salaam wakati wengine hususani wale wa timu ya Azam FC walichukuliwa na
viongozi wao kwa ajili ya safari ya kwenda Mbeya ambako Jumatano wanatarajiwa
kucheza na Tanzania Prisons kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara
utakaofanyika Uwanja wa Sokoine mjini humo.
Kadhalika wachezaji wa Young
Africans nao walichukuliwa kwa ajili ya safari ya kwenda Mtwara ambako watakuwa
na mchezo dhidi ya Ndanda FC kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini humo
wakati nyota wa Simba watabaki hapa Dar es Salaam kwani Jumatano itakuwa na
kibarua dhidi ya Ruvu Shooting kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom.
Wakati nyota 18 wakitua Dar es
Salaam, Nahodha wa timu hiyo, Mbwana Samatta aliishia Nairobi, Kenya ambako
aliunganisha ndege ya kwenda Brussels, Ubelgiji.
Licha ya mchezo huo kuwa sehemu
ya mchuano wa kuwania nafasi ya kucheza fainali hizo za AFCON 2017 huko Gabon,
lakini ulikuwa ni wa kukamilisha ratiba baada ya Misri kufuzu kwa fainali hizo
kutoka kundi G ambalo mbali ya Nigeria na Tanzania, pia ilikuwako Chad ambayo
iliyojitoa katikati ya mashindano.
No comments