WACHEZAJI WA YANGA WANA DENI KUBWA.

Na Richard Leonce.

Kwa siku za hivi karibuni, Klabu ya Yanga imekua mfano wa kuigwa katika suala zima la kuiandaa timu yao. Hapa ni lazima tuseme ukweli kwamba wanstahili pongezi.


Kuanzia kwenye maandalizi ya msimu uliomalizika kama utakumbuka Yanga walikua kati ya timu zilizoanza kambi mapema sana. Tena baadhi ya wachezaji nakumbuka walikua kwenye majukumu ya timu ya taifa, lakini Yanga wakaingia kambini wakitumia uwanja wa Karume wakaanza mazoezi yao kwa umakini na matokeo yake wote tumeyaona.

Unaweza kuulaumu uongozi wa Yanga kwa mengine ya nje ya uwanja huku, lakini kwa suala la maandalizi ya timu wapo vizuri sana. Kitu ambacho nina ushahidi nacho ni jinsi wanavyompa nafasi mwalimu wao Hans Van Pluijm kufanya kazi yake. Wote tunakumbuka huko nyuma kulivyowahi kuwa na vichekesho vya makocha kupangiwa vikosi. Naweza kukuhakikishia kwamba Yanga imekua kituo cha mabadiliko katika hilo.

Hata katika usajili, tumeona Yanga wakiwa na makosa machache tofauti na zamani. Japo bado wana usajili wa kumzodoa mtani, lakini bado hawaachi kutekeleza anachotaka kocha. Na kocha wao nae hana hiyana kwa kweli, anatoa nafasi kwa wachezaji wenye uwezo wa kuisaidia timu. Kwa ufupi kwa hapa nchini, Yanga wanayafanya mambo yao ipasavyo.

Napenda wachezaji wa Yanga watambue haya. Wapo ambao hawajui hali ilikuwaje huko nyuma lakini wapo wanaotambua. Watu kama Calvin Yondani, Deogratius Munish, Nadir Haroub na Ali Mustafa wanajua machungu ya hizi timu kubwa ambayo sasa hivi yamepungua kwa upande wa Yanga.

Wachezaji wanapaswa kujua kwamba kila kinachofanyika kwa ajili yao kinapaswa kulipwa kwa ushindi. Watu sasa hivi wanataka ushindi na siyo tena kiwango cha kuvutia.

Unapewa kambi ya gharama kubwa Uturuki ambayo pamoja na maneno mengi lakini kocha Hans ndiye aliiomba na uongozi ukampatia. Unapaswa kuijibu kwa ushindi. Haina maana kama unapewa kila unachohitaji halafu unafungwa mechi mbili mfululizo ikiwemo moja ya nyumbani.

Miaka ya nyuma wachezaji walikua wanasingizia kutoandaliwa, na kweli kwa viwango vyao na mioyo yao inawezekana walikua sahihi, lakini leo wachezaji wa Yanga mmeandaliwa vizuri, wapeni raha mashabiki wenu.

Mna kikosi bora kabisa lakini hiyo haitoshi, mnapaswa kujituma kupita kawaida ili kushinda michezo hii ya kimataifa. Huku hakuna anaemjua Tambwe wala Ngoma kusema atamwogopa kwa jina lake na ndiyo maana hata kasi ya ufungaji kwa washambuliaji wa Yanga imepungua sana. Wanaaswa kushusha mabega na kufanya kazi kama watumwa kwa dakika 90.

Mabeki wa Yanga pia wazingatie wanachofundishwa. Tatizo kubwa ni kwamba kwenye mechi nyingi za ligi kuu, Yanga ilikua haipati upinzani wa kutisha hivyo mabeki wao wakajiamini kupita kiasi. Mabeki wa Yanga walikua hawaamini kama wanaweza kutikiswa na zaidi wakawa wanawaza kushambulia tu. Sasa huku kwenye michuano ya kimataifa hakuna hayo.

Utaona magoli mengi wanayofungwa yanatokana na mipira ya kutengwa, tena wakati mwingine dakika chache kabla ya mpira kumalizika. Sasa wanasema kutenda kosa si kosa lakini unapofungwa magoli yanayofanana zaidi ya mara mbili au tatu hapo kuna shida ya kiufundi.

Mimi sina shida sana na mwalimu Hans, amekwishauthibitisha ubora wake na nimemshuhudia mara kadhaa kwenye mazoezi ya Yanga akisisitiza mambo yote muhimu. Deni langu mimi lipo kwa wachezaji. Mna uongozi mzuri unaowajali, mna kocha mzuri mwenye mbinu nyingi, mnalipwa pesa nzuri zaidi ya timu nyingi kwenye ukanda huu, mna vipaji. Hebu onyesheni basi kwamba mnastahili kuwa hapo mlipo. Sitowaelewa kama hata Medeama atashindwa kufungika tena hapa nyumbani.

Mna jukumu kubwa la kukonga nyonyo, Mashabiki wenu hawajazoea kufungwa na mkiendelea kuwazoesha hawatochelewa kuwageuka, si mnajua wenyewe mpira wetu ulivyo?
Mungu Ibariki Yanga...
Mungu Ibariki Tanzania...

0766399341

No comments

Powered by Blogger.