THE GUNNING MACHINE : HATA MIMI NINGEKUA HENRY NINGEONDOKA ZANGU.

Na Richard Leonce

Ni siku ambazo mashabiki wengi wa Arsenal hawana cha kujivunia kwa kweli. Timu haitambi kwenye soko la usajili lakini hata ukiangalia wachezaji walioko sokoni huoni tiba ya matatizo ya Arsenal ikikaribia kufika.



Nilikua nachekeshwa na taarifa moja hapa eti Napoli wamesema ili wamwachie Gonzalo Higuain inabidi Arsenal wafanye biasharabya kubadilishana na Olivier Giroud. Nimecheka sana.

Baniani mbaya kiatu chake dawa. Ni nani anatamani Giroud aondoke?
Bado najisikia kuendelea kumkosoa akiwa Arsenal na sijisikii kumwona akiondoka leo wala kesho. Napoli kama biashara ndo hiyo bakini na Muargentina wenu, tuache na Mfaransa wetu.

Arsenal imemsajili Takuma Asano.
Sina cha kusema hapa kwa sababu mbili. Kwanza simjui, sijapata kumwona akicheza. Pili, ni kipi utaongea kama timu yako inasajili mjapan aliyefunga magoli 11 katika michezo 56? Sana sana unaweza kuuponda usajili huo.

Moja kati ya habari za kusikitisha sana zilizonifikia ni hii ya kuondoka kwa Thierry Henry. Imenihuzunisha kama nilivyohuzunika miaka kumi iliyopita wakati Henry akiwa mchezaji alipohamia Barcelona. Leo ninahuzunika tena Henry akiondoka kama kocha wa vijana.

Unaweza usifahamu, lakini Henry amekuwepo Arsenal kwa miezi kama 18 hivi huko Academy akifundisha. alianza kwa kufundisha vijana wa chini ya miaka 15 kabla hajapandishwa October mwaka 2015 kufundisha vijana wa chini ya miaka 18 alipopata beji yake ya ukocha kutoka UEFA.

Ilikua ni habari njema sana kwangu. Mimi huwa naiota ndoto fulani ya kipuuzi ya kuiona Arsenal chini ya Denis Bergkamp na Thierry Henry kama kocha mkuu namsaidizi wake. Kitendo cha Bergkamp kuwa msaidizi wa Frank De Boer kule Ajax na Henry kuwa kwenye Academy ya Arsenal kilikua kinaiweka hai ndoto yangu lakini sasa ni kama nimeshtuliwa kutoka usingizini wakati ndoto ikiwa ndo inaelekea kuanza.

Henry ameamua kuondoka na sina woga wa kusema kwamba aliyemwondoa ni Arsene Wenger. Kwanza nilianza kusikia habari za chini chini kwamba Henry anataka kuwa juu ya kocha Kwame Ampadu ambaye anakinoa kikosi cha vijana tangu mwaka 2012, nikashangazwa na hilo kwa sababu lilikaa kama propaganda. Kwame ndiye aliyempokea Henry kwenye Academy na walikua wakifanya kazi kwa ukaribu sana.

Lakini sasa ukweli umekuja wazi. Imebainika kwamba kinachomwondoa Henry ni sharti la Bosi Arsene Wenger la kumtaka Henry aache kazi ya uchambuzi pale Sky Sports kama anataka kuingia moja kwa moja kwenye benchi la Arsenal. Kuna mengi nyuma ya huu uamuzi.

Natambua kwamba suala la nani afundishe vijana wa chini ya miaka 18 si kubwa sana, lakini nakumbuka Henry hajaanza uchambuzi leo. Alianza uchambuzi akiwa kocha wa vijana wa chini ya miaka 15 Arsenal japo hakua 'official' kwa sababu alikua bado hajapata beji ya UEFA. Taarifa iliyopo ni kwamba Andries Jonker ambaye ni meneja wa Academy ya Arsenal ndiye aliyemuahidi Henry kwamba akipata beji yake basi ataendeleza maisha yake ya ukocha akiwa na Arsenal.

Najiuliza ni kwa nini Henry hakuonywa wakati anasaini deal la uchambuzi na Sky Sports kwamba lingehatarisha maisha yake ndani ya Arsenal? Badala yake Arsene Wenger akampongeza.

Hivi unamwambiaje mtu aache kazi ambayo inamlipa Pauni Milioni 4 kwa mwaka?
Tena mtu ambaye ni mchezaji mstaafu. Hili ni sharti ambalo lingeweza kutekelezeka enzi za akina Nuhu. Katika dunia ya leo hata Arsene Wenger mwenyewe angekua ndiyo Henry asingekubali.
Hii dunia ambayo Ronaldinho Gaucho anacheza mechi maalumu ya kujipatia pesa, pesa imekua ngumu wakati ikiwa ndiyo kila kitu.
Hata mimi ningekua Henry ningeaga vizuri tu.

Habari inayonihuzunisha ni kwamba Sky Sports walimruhusu Henry akafundishe Arsenal, na Henry alikua tayari kufundisha bure kwa sababu analipwa vizuri na Sky. Inawezekana unashangaa kwa nini mimi nasikitika sana Henry kuondoka. Nasikitika kwa sababu najua Henry ni mfalme, ni mtu ambaye wale vijana wa Academy wanamuhitaji sana zaidi ya makocha wengine. Labda kitu kizuri ni kwamba nimesikia Ian
Wright ndiye atakayechukua nafasi hiyo.

Labda kwa nini nakua na wasiwasi na uamuzi huu. Ni kile kinachotajwa kwamba maneno ya Henry kwamba Arsenal haitotwaa ubingwa kama striker wake ni Olivier Giroud yalimuudhi Wenger. Inasemekana ndiyo chanzo cha yote haya. Wenger anaweza kuwa na lengo zuri la kutohitaji mtu asiyeamini katika mipango yake kwa sababu pengine uwepo wa Henry unaweza kuondoa hali ya kujiamini kwa kikosi ambacho straika wake ni Olie.

Lakini kwa upande mwingine, Henry hakusema uongo jamani. Siyo rahisi kutwaa ubingwa kama Olie ndiye mshambuliaji wako namba moja.

Sasa kitakachotokea kibaya ni kwamba Henry ataenda kufundisha timu nyingine. Masharti ya beji ya UEFA yanamtaka afundishe kama anataka kuendelea kuwa nayo. Tunaweza kuwa tumempoteza Henry kama tulivyowapoteza akina Patrick Vieira na Denis Bergkamp ambao wanalisha vilabu vingine.

Hivi karibuni tumempoteza Mikel Arteta tena kwa adui. Usitegemee Arteta atashindwa kuuza siri za Arsenal kwa mwajiri wake mpya pindi tutakapokutana. Tukutane juma lijalo.

0766399341

No comments

Powered by Blogger.