KOCHA MPYA AZAM AANZA NA USHINDI

KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Zeben Hernandez, jana ameiongoza timu hiyo kwenye mchezo wa kwanza tokea akabidhiwe mikoba hiyo kwa kuichapa Ashanti United mabao 2-0.


Mchezo huo wa kirafiki wa kujiandaa na msimu ujao ulifanyika saa 3 asubuhi ndani ya dimba la Azam Complex, ambapo Zeben alipata fursa ya kukifanyia tathimini kikosi chake baada ya kuchezesha vikosi viwili tofauti kwenye kila kipindi cha mechi hiyo.

Ikiwa imefanya mazoezi kwa siku tisa chini ya makocha wapya kutoka Hispania, Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB ilijitahidi kumiliki mchezo huo, lakini ilishindwa kutumia nafasi takribani tano ilizotengeneza za kufunga mabao, ambapo ilishuhudiwa ikimaliza kipindi cha kwanza ikiwa imetoshana nguvu ya bila kufungana na wapinzani wake hao.

Mabadiliko ya kipindi cha pili aliyofanya Zeben ya kuingiza kikosi kingine, yazidi kuipa uhai zaidi Azam FC na hatimaye ikaweza kufunga mabao mawili mazuri ya kiufundi kupitia kwa viungo Mudathir Yahya na Abdallah Masoud ‘Cabaye’.

Mudathir ndiye aliyeanza kuziona nyavu za Ashanti United akifunga bao zuri dakika ya 69 kufuatia pasi safi ya Frank Domayo na kupiga shuti kali akiwa ndani ya eneo la 18 pembeni lililomshinda kipa Rajabu Hamisi.  

Cabaye alihitimisha ushindi huo kwa kufunga bao safi la pili akitumia vema pasi ya Ame Ally ‘Zungu’ dakika ya 81 na kupiga shuti kali akiwa umbali wa takribani mita 20 lililojaa wavuni na kuifanya Azam FC kuondoka na ushindi huo.

Katika mchezo huo benchi la ufundi la Azam FC lilipata fursa ya kuwajaribu wachezaji wawili waliokuwa majaribio, kipa Mhispania Juan Jesus Gonzalez aliyefuzu majaribio na mshambuliaji kutoka Ivory Coast, Ibrahima Fofana, ambao wote walicheza kipindi cha kwanza kabla ya timu nzima kubadilishwa kipindi cha pili.

Zeben aizungumzia mechi

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabuwww.azamfc.co.tz mara baada ya mchezo huo, Zeben ameeleza kufurahishwa kwa namna mchezo huo ulivyochezwa na viwango vya wachezaji wake, lakini hajafurahishwa na namna alivyowakosa baadhi ya nyota wake.

“Nimefurahishwa na viwango vya wachezaji wangu naamini itapelekea Azam FC kuwa na ubora mwakani, sijafurahishwa kuwakosa baadhi wachezaji wangu kama vile Shomari Kapombe (mgonjwa), Pascal Wawa (majeruhi) Kipre Tchetche na Farid Mussa anayeenda Hispania,” alisema.

Kocha huyo wa zamani wa Santa Ursula ya Hispania alisema kuwa amewaachia viongozi wa Azam FC kuhakikisha wanaziba mapengo hayo haraka iwezekanavyo, ambapo hivi sasa uongozi wa timu hiyo upo kwenye mchakato huo.

Mabao si ‘ishu’ hivi sasa  

Zeben alisema kwa sasa wanajaribu kuunda timu hiyo kwa kutatua matatizo yaliyopo kikosini, huku akidai kuwa katika mchezo wa leo walikuwa hawaangalii mabao bali eneo la ulinzi pekee na namna wachezaji wanavyocheza kwa nafasi.

“Tulikuwa tunaangalia eneo la ulinzi kwenye mchezo huu, tulikuwa hatuangalii sana mabao, mabao yalikuja kama kitu cha ziada tu, bado tupo kwenye kuunda timu na nasubiria uongozi ufanyie kazi mapengo hayo baada ya baadhi ya wachezaji kutokuwepo kikosini,” alisema.

Itamchukua mwaka wachezaji kuzoea mfumo

“Inaweza kuchukua mwaka mzima wachezaji kuuushika na kuuzoea mfumo wangu, kwa sasa tunaifanyia kazi Azam FC na wachezaji ni Azam FC, tunachofanya hivi sasa ni kupandikiza vitu vipya tulivyokuwa navyo kwa wachezaji taratibu kwa sababu wachezaji nao ni watu na huwezi kuwapa dozi kubwa.

“Itawachukua muda kidogo kuweza kuzoea falsafa yetu, kwani tupo kwenye kuivunja falsafa ya Uingereza waliyokuwa wanatumia msimu uliopita na kuingizia yetu ya Hispania, hivyo itachukua muda lakini ndicho tunachokifanyia kazi sasa hivi,” alisema.

Azungumzia majaribio ya Fofana, Gonzalez

Kocha huyo, 32, alisema kuwa Fofana si mchezaji mbaya kwa namna alivyomuaona kwenye mchezo wa leo huku akidai kuwa anahitaji kumwangalia zaidi katika muendelezo wa majaribio yake wiki ijayo inayoanza kesho Jumatatu.

“Kwanza ana heshima, anajifunza haraka anashirikiana vema na wenzake, lakini uamuzi zaidi wa majaribio yake utakuja wiki ijayo, lakini kwa sasa si mbaya,” alisema.

Zeben aliweka wazi kuhusiana na majaribio ya makipa Juan Jesus Gonzalez na Daniel Yeboah kutoka Ivory Coast, akidai kuwa Mhispania huyo amefuzu majaribio jana huku akimwelezea kuwa ni kipa mwenye kipaji kikubwa, ana mbinu kubwa na uwezo mkubwa wa kufikiri.

“Naamini ya kuwa kuwepo kwake kwa kushirikiana na makipa wengine, Azam FC itakuwa sehemu nzuri kwenye nafasi za juu na kudai kuwa makipa wote ni wazuri,” alisema.

Alisema kuwa ingekuwa ni uwezo wake angeweza kumchukua na kipa mwingine Yeboah aliyefeli majaribio, lakini kutokana na kuhitajika kwa nafasi moja ya kipa wa kigeni ameamua kumchagua Juan Jesus Gonzalez, huku akisisitiza kuwa makipa wote hao ni wazuri.

Baada ya mchezo huo wa kwanza wa kirafiki, Azam FC inatarajia kushuka tena dimbani Jumatano ijayo saa 3 asubuhi kuvaana na timu ya Halmashauri ya Kinondoni (KMC) kwenye mechi nyingine ya kujipima ubavu.

Kikosi cha Azam FC

Juan Jesus Gonzalez/Aishi Manula dk 46, Wazir Salum/Gadiel Michael dk 46, Erasto Nyoni/Abdallah Kheri dk 46, Aggrey Morris/Ismail Gambo dk 46, David Mwantika/Himid Mao dk 46, Michael Bolou/Frank Domayo dk 46, Jean Mugiraneza/Mudathir Yahya dk 46/Himid Mao dk 77, Salum Abubakar/ Abdallah Masoud ‘Cabaye’ dk 46, Ramadhan Singano/Khamis Mcha dk 46, Ibrahima Fofana/Kelvin Friday dk 46, Shaaban Idd/AmeAlly dk 46.

..Source : www.azamfc.co.tz

No comments

Powered by Blogger.