THE GUNNING MACHINE; NYOTA WA ARSENAL KIMATAIFA, USAJILI NA MENGINE YANAYOENDELEA KLABUNI.

Na Richard Leonce

Granit Xhaka amefanya ziara kwenye uwanja wake mpya wa nyumbani wa Emirates na uwanja wa mazoezi wa Colney juma hili. Hii ni baada ya mkwaju wake wa penalt kuota mbawa na kuipeleka nje ya mashindano ya Euro timu yake ya taifa ya Switzeland. Katika mchezo huo dhidi ya Poland ulioamuliwa kwa mikwaju ya penalt, ni Xhaka pekee aliyekosa.



Nilipata hamu ya kujua yeye mwenyewe amechukuliaje jambo hilo. Anasema wala haijamyumbisha, sana sana imemfanya akomae kama mwanasoka.
Safi, ndivyo inavyopaswa kuchukuliwa. Matukio ya kukosa penalt muhimu huwatokea sana wanasoka, na wote tunajua hata Lionel Messi alikosa mkwaju ambao uliinyima Argentina kombe la Copa America.

Saa chache baada ya penalt ya Xhaka kuongezeka kasi, Mesut Özil nae akapata penalt kwenye mchezo dhidi ya Slovakia. Sijui Wajerumani walizingatia nini kumpa Özil mkwaju ule kwa sababu hana historia nzuri sana na mikwaju hiyo. Kwa mara nyingine tukamshuhudia akiupeleka mpira kwenye mikono ya golikipa.
Nadhani tukubaliane tu kwamba Özil si mpigaji mzuri wa Penalt.

Kwenye Copa America, Alexis Sanchez ameng'ara kweli kweli. Pamoja na kuiwezesha timu yake ya Chile kutetea ubingwa wa michuano hiyo wakiwashinda Argentina kwa mikwaju ya penalt kwa mara ya pili mfuatano, Alexis ameondoka na tuzo ya mchezaji bora wa michuano hiyo.
Siyo jambo dogo kubeba tuzo hiyo kwenye michuano ambayo imewahusisha pia akina Lionel Messi, James Rodriguez, Arturo  Vidal, Sergio Aguero na wengineo. Sanchez anastahili pongezi.

Kwenye usajili huku, tayari Jamie Vardy ameshanifanya mjinga, nilihisi hiki kitu mapema lakini nikawa mgumu kuamini. Vardy ameamua kusalia kwenye klabu yake ya Leicester. Tumekosa kitu, lakini si kikubwa sana. Nadhani mahitaji yetu kwa Vardy yalikua 50/50 sawa na ambayo Vardy alituhitaji sisi. Kwa umri wake na aina ya mkataba ambao ilitajwa kwamba Arsenal ingempa, ni sawa na mtu kupiga teke fuko la dhahabu.

Sasa tumebaki kwenye yale maisha yetu ya kawaida tu ya tetesi. Tetesi zile zile kama zilivyowahi kuvuma kwa akina Gonzalo Higuain, Juan Mata, Eden Hazard, Jesus Navas, Julian Draxler, Stevan Jovitec n.k
Mara nyingine hili la Vardy halishangazi sana kwa sababu walau tulijua kwamba tunamsubiri afanye maamuzi, na amefanya maamuzi yake.

Nilikua napita mtandaoni nikakutana na habari kwamba Wasaka vipaji wa Arsenal wameweka lengo la kumsajili Mjapan anaitwa Asano Takuma. Najua unasonya kwa sababu humjui, hata mimi simjui. Labda tutamwona kwenye Olympic.
Nasikia tu ni mshambuliaji, si jambo baya kuongeza mtu kikosini. Nani anajua labda anaweza kwenda mahali kwa mkopo kisha akageuka Joel Campbell mpya.

Si vizuri kumwongelea wakati hata mchakato wa kumsajili haujafanyika, lakini tukubaliane tu kwamba huyo hatokua tiba ya matatizo yetu kwa sasa. Hiyo ndiyo sababu tunahusishwa pia na tetesi za kumsajili Alexandre Lacazette kutoka Lyon ya Ufaransa.

Ni mwaka wa tatu sasa nasikia tunamvizia Lacazette lakini hilo siyo tatizo. Tatizo ni kwamba, Lacazette ndiye aina ya mshambuliaji tunayemtaka? Natambua kwamba wengi tunamtaka mshambuliaji ambaye atamfanya Olivier Giroud awe chaguo la pili kikosini, lakini mimi najua mtu huyo hawezi kua Lacazette.

Lacazette na Giroud ni kama pipa na mfuniko, hawana tofauti kubwa, tena Giroud anaweza kua bora zaidi.
Alikua mfungaji bora wa League 1 kwenye msimu wa 2014/2015 akifunga mabao 27 kwenye michezo 33, lakini msimu uliopita amefunga mabao 21 kwenye michezo ile ile 33.
Huyu si mtu wa kumsumbua sana Giroud.

Haoneshi kama grafu yake inapanda na ndiyo maana Wafaransa wenyewe hawaoni sababu ya kumjumuisha kwenye kikosi chao cha Taifa. Lakini pia ukimtaka Lacazette sasa hivi ujipange, unadhani atauzwa kwa bei gani wakati hata PSG wanamtaka.

Kama unaambiwa Michy Batshuayi ana thamani ya £40 milioni unadhani Lacazette atakua na thamani gani?
Batshuayi amefunga mabao 17 kwenye League 1, Lacazette amefunga 21 na yupo kwenye nafasi ya pili nyuma ya Zlatan Ibrahimovic.

Hapo ndipo Mzee wangu Arsene Wenger anapoamua kuweka pamba masikioni kwa sababu kutoa £50 Milioni kwa ajili ya Lacazette wakati una Giroud kikosini inahitaji ukarimu wa hali ya juu ambao Wenger hana. Tuvute subira tutaona mwisho wake.

Zaidi ni kwamba kikosi chetu cha Vijana wa chini ya miaka 21 tayari kimeanza kambi, natarajia wawili watatu tutawaona kwenye kikosi cha kwanza kama akina Dan Crowley, Chris Willoc, Krystian Bielik au pengine ukawa msimu wa bahati kwa Gidion Zelalem. Sitaki kumsahau Stephy Mavididi ambae alionesha kiwango bora kabisa msimu uliopita.

0766399341
Twitter. @chardboy77

No comments

Powered by Blogger.