THE GUNNING MACHINE : WENGER ANATUPIKIA MCHUZI GANI?
Na Richard Leonce
Wasomaji wangu wa TGM waliikosa hii makala ambayo ilikwishaanza kusambaa mioyoni mwao kwa kipindi kirefu sana. Si nia yangu leo kueleza sababu za kuacha kuandika TGM, tutaziongea siku nyingine.
Leo nimeamua kuandika baada ya msimu kumalizika tukiwa katika nafasi ya pili kwenye msimamo.
Uso wangu sio wenye bashasha ingawa kihesabu na kitakwimu tutasema msimu uliokwisha ulikua wa mafanikio.
Ndiyo tulipoteza kombe la FA, tena natema mate kwa hasira nikigundua tumelipoteza kwa Manchester United.
Lakini kwa upande mwingine, hii nafasi ya pili hii tulikua hatujaipata tangu msimu wa 2004/5.
Yaani tumesubiri kwa miaka 10 kuingia kwenye Top 2. Basi tuyaite mafanikio.
Nikitazama nyuso za mashabiki wa Arsenal naziona zikitamba kwa jeuri kwamba Arsenal haikupaswa kumaliza chini ya Leicester, tena kwa pointi 10. Hii jeuri wanayo sana mashabiki wa Arsenal kama akina Heavy D.
Eti wanapata jeuri hii kutokana na kua timu pekee iliyomfunga Leicester nyumbani na ugenini.
Ni kweli, lakini Leicester wanaweza kutucheka kwa dharau kwa sababu bado tulichemka mbele ya watu kama Chelsea, Southampton, West Brom nk.
Yani ni sawa na Coastal Union hapa nchini atambe kwamba alimfunga bingwa Yanga, lakini akashuka daraja. Haitofautiani sana.
Wakati msimu ukielekea mwishoni, Kocha kipenzi Arsene Wenger akapata changamoto ya nguvu sana katika maisha yake. Makaratasi meupe kutoka kwa mashabiki yakaanza kumwandama yakimtaka aachane na timu hiyo ambayo amekaa nayo mpaka akafanana nayo kwa kila kitu.
Mashabiki wengi mashuhuri wa Arsenal hawataki tena kumsikia Wenger, na wanateswa sana na ukweli kwamba Mzee huyo bado atakua nao kwa msimu mwingine.
Swali gumu likiwa ni je atawezaje?
Wenger amekwishapoteza imani ya wapenzi, sijui kwa wachezaji hasa wakubwa ambao wanajua hasa ni wapi anakosea. Lakini ukweli ni kwamba si jambo zuri kupoteza imani ya mashabiki wako kwako.
Sasa namtazama mzee wangu huyu akianza kuupika rasmi mchuzi wake ambao amekua akiupika kwa misimu kadhaa.
Msimu huu ana kazi kwa sababu ni lazima awaaminishe walaji kwamba mchuzi huo ni tofauti kwa ili wao washawishike kuuonja.
Vinginevyo hawatauonja na hiyo itakua ni hasara kubwa sana.
Arsena ni timu ya wafanyabiashara, tena wengine wala si wapenzi wa soka, wao ni wapenzi wa biashara tu.
Katika hali hii ambayo mashabiki wa Arsenal wameonesha kuja juu, kumkataa kocha ambae bado anang'ang'ania kumaliza mkataba wake, ni lazima akili ya biashara itume, na bahati nzuri Wenger anaiweza sana, na amekwishaanza.
Nimeona jezi mpya za nyumbani msimu huu. Jezi zimezinduliwa na zimetumika kutuma ujumbe mzito kwa mashabiki wa Arsenal kuisapoti timu yao.
Naona picha ya jeshi kubwa la mashabiki wa Arsena likiwa nyuma ya wachezaji. Hali ambayo Arsene Wenger amekua akiisisitiza sana.
Kama haitoshi, mapema kabisa Wenger anaingia sokoni kununua mchezaji, huyu si Wenger wa kawaida huyu.
Anamnunua Granit Xhaka kutoka Borussia Monchenglandbach wakati huu kwa sababu tatu,
Kwanza anahitaji kupanua kikosi chake baada ya kuondokewa na viungo watatu kwa mpigo. Hawa ni Thomas Rosicky, Mathieu Flamini na Mikel Arteta.
Pili, anaomba jamvi mapema kabla hawajaomba wenzake.
Hataki kumtaja taja mtu kwa sababu mara nyingi afanyapo hivyo, watu humwibia mawazo yake.
Tatu ambayo ndiyo muhimu, anataka mashabiki waanze kumzungumzia zaidi Xhaka wanapoitaja Arsenal kwa sasa badala ya kumzungumzia yeye kwa sababu hawana zuri la kuzungumza.
Wapo akina Festo Kalawa ambao wana mazuri ya kumwongelea Wenger, lakini ni punje chache sana zisizoiva kwenye pishi la choroko.
Kuruhusu watu wamwongelee Wenger kwa sasa ni kutengeneza mpasuko, na ndiyo maana Wenger na bodi ya Arsena kwa makusudi hawataki kuruhusu hilo.
Kwa namna nyingine, msimu ujao kwa Arsenal unaweza kuwa wa maandalizi ya timu kwa mrithi wa Arsene Wenger, japo naamini Wenger atataka bakshishi kwa ajili ya Send Off, lakini siwezi kumwambia shabiki wa Arsenal atarajie msimu mzuri zaidi ya mingine.
Kitu cha kutarajia ni usajili kuendelea, Usajili ambao unaweza ukawa mkubwa kama wa Ozil, au usajili ambao vyombo vya habari vya Uingereza vitatuambia ni mkubwa kama huu wa Xhaka.
Kwani nani alikua anamjua Xhaka kama anavyomjua sasa hivi?
Ni lazima Wenger atupe sababu ya kuusubiri msimu ujao, ni lazima awafanye mashabiki wanunue tiketi kwa bei kubwa, hiyo ndiyo kazi yake kubwa zaidi ya kuleta vikombe.
Na wenger ni mzuri zaidi kwenye hilo kwa sababu bado ana uhakika wa kukupa matokeo mazuri kiasi hasa kwenye ligi ya nyumbani.
Nausubiri mchuzi wa Wenger, najua utakua mtamu lakini wa aina ile ile. wa kuziba pasipovuja sana na kupaacha panapovuja sana.
Wakati dirisha la usajili linafungwa mwaka 2015, Wenger alimsajili golikipa Petr Cech pekee na akatubishia tuliposema alihitaji wachezaji wengine zaidi ili akamilike.
Ni kweli akatuonesha akina Alex Iwobi lakini walichompa ni kile tulichokitarajia.
Hebu tukutane juma lijalo tuangalie anachokuja kuongeza Granit Xhaka kwenye eneo letu la kiungo. Tuendelee kuusubiri mchuzi wetu uive.
0766-399341
No comments