SIMBA YARUDI TENA KILELENI MWA MSIMAMO, HAMIS KIIZA AMLIPA TAMBWE

Wekundu wa msimbazi Simba wamerudi tena katika kilele cha msimamo wa ligi kuu Tanzania bara baada ya kuifunga Ndanda FC ya Mtwara kwa bao 3-0 jioni hiI.




Mchezo huo wa ligi kuu Tanzania bara ulipigwa katika dimba la Taifa jijini Dar es Salam na mpaka mapumziko tayari Simba walishakua mbele kwa bao 1-0 goli lililofungwa na Kiungo wa timu hiyo Mwinyi Kazimoto akitumia vyema mpira wa krosi ya Ibrahim Ajib toka upande wa kulia wa uwanja mpira uliowapita mabeki wawili pamoja  na kipa wa Ndanda na kumwacha Kazimoto akiwa peke yake.

Kipindi cha pili kilikua faraja kwa mshambuliaji Raia wa Uganda Hamis Kiiza baada ya kuifunga Simba mabao mawili la kwanza akifunga kwa kichwa baada ya kuunganisha mpira wa kona huku lile la pili akifunga baada ya kipa wa Ndanda kushindwa kudaka mpira uliopigwa na Justice Majabvi kisha Danny Lyanga kumwekea Kiiza ambaye alifunga bila kutumia nguvu.

Kwa matokeo hayo Simba sasa wanaishusha tena Yanga kileleni kwani inafikisha pointi 51 pointi moja mbele ya Yanga wenye pointi 50 katika nafasi ya pili japokua Simba imecheza michezo 22 na pia Hamis Kiiza nae anarudi juu katika orodha ya wafungaji bora akiwa na magoli 18 goli moja zaidi ya Amiss Tambwe mwenye magoli 17 ambaye juzi alifunga magoli mawili pia.

Katika mechi nyingine leo ya ligi hiyo Mbeya City wakiwa katika uwanja wao wa nyumbani kule Mbeya waliifunga Stand United toka Shinyanga kwa bao 2-0.

No comments

Powered by Blogger.