RAIS WA FIFA AKARIBISHWA KWA MECHI, ADAI MPAKA SASA HAJUI ATAPOKEA MSHAHARA KIASI GANI

Rais mpya wa FIFA Gianni Infantino amekaribishwa ofisini kwa mechi ya mpira wa miguu na wakongwe waliowahi kuwika katika soka duniani huku yeye akiwa ni nahodha wa timu mojawapo na kuvalia jezi namba 9.




Katika mechi hiyo Infantino Alitaka kuonyesha ulimwengu kwamba sasa FIFA ni kwaajili ya maendeleo ya mpira wa miguu (Soka) na yote yaliyopita na kupelekea kusimamishwa viongozi  wa Shirikisho hilo yanapaswa kuwekwa kando na ni muda sasa wa kuendeleza soka duniani ndiyo maana yeye naye akacheza katika mechi hiyo.

Katika mechi hiyo ambayo timu aliyochezea Infantino ilifundishwa na kocha wa zamani wa England Fabio Capello walishiriki pia magwiji wa soka wa zamani wakiwemo Luis Figo, Demetrio Albertini, Zvonimir Boban, Fabio Cannavaro, Paulo Maldini, Deco, Fernando Hierro, Robert Pires, Clarence Seedorf, Andriy Shevchenko na Kelly Smith.

Gianni Infantino pia alitanabaisha kuwa mpaka sasa hajui atapokea mshahara kiasi gani kwani hajaongea na mtu yeyote kuhusu swala la mshahara wake kama Rais wa FIFA  na kusema hata alipokua akigombania nafasi hiyo mawazo yake hayakua kuhusu mshahara bali  kuendeleza soka.

Gianni Infantino alichaguliwa hivi karibuni kama Rais mpya wa Shirikisho la Soka duniani FIFA akichukua nafasi ya Sepp Blatter aliyefungiwa kujihusisha na maswala yote yahusuyo soka kutokana na kukumbwa na kashfa ya Ufisadi katika chombo hicho chenye mamlaka ya juu kabisa katika soka duniani.

No comments

Powered by Blogger.