LVG UMEISHINDWA UNITED,RASHFORD NA WENZIE NI KIVULI TU CHA MUDA MFUPI
Majuma kadhaa yaliyopita jina la LVG kwa mashabiki wa Man Utd lilikuwa chungu kuliko tamu na wengi wao walikuwa hawamtaki mkufunzi huyo wa kidachi kuendelea kukinoa kikosi hicho, wakiamini kuwa ameshindwa kuirejesha timu pale wengi walipotarajia hata baada ya kutumia pesa nyingi katika madirisha makuu mawili ya kiangazi.
Pamoja na kuwa na majeruhi wengi wa kikosi cha kwanza lakini hata alipokuwa na wachezaji hao bado mwenendo wa timu hiyo haukuwa wa kuridhisha huku ikicheza mpira wa taratibu na usiovutia machoni mwa mpenzi yeyote wa soka achilia mbali shabiki wa United.Lakini bahati nzuri kwake katika siku za usoni majina ya Rashford, Varela, Fosu na makinda wengine waliopata nafasi na kuonesha uwezo wao yamewasahaulisha wapenzi wa United kuwa LVG bado ni yule yule anayeshika nafasi ya 6 kwenye ligi kwa sasa, vile vile ni yeye ambaye ameitoa timu UCL hatua ya makundi pia ndio huyu huyu aliyekifanya kiungo cha United kiwe na machaguo mengi huku eneo la ulinzi na lile la kushambulia yakiwa kama debe tupu tu huku akijua wazi timu ina mashindano mengi tena magumu ya kushiriki.
Matokeo yake Blind,Young, Carrick wamekuwa wakitumika kama viraka kwa nyakati tofauti kuziba mashimo kwenye eneo la ulinzi msimu huu pia akithubutu hata kumtumia Fellaini kama mshambuliaji wakati fulani huku Javier Hernandez akionesha thamani yake kule Ujerumani na kile ambacho LVG alikikosa baada ya kukitupa na bado anaendelea kukikosa hata baada ya kuibuka ghafla kwa Marcus,pia LVG ndio huyu huyu aliyeirudisha timu UCL kisha kuipeleka ikacheze usiku wa ulaya siku za alhamisi na ni yeye pia aliyeshindwa kuishi vyema na kipaji cha ADM msimu ulioisha huku Laurent Blanc akifaidika na ujio wake pale PSG msimu huu.
Kamwe simdharau kwa alichokifanya LVG na mchango wake mkubwa katika soka sanjari na kuibua vipaji vya vijana mbalimbali vilivyokuja kuwa tishio baada ya kuwaamini na kuwapatia nafasi,Tabu yangu na yeye inakuja kwenye sera yake ya usajili pamoja na hicho anachokiita falsafa ndani ya miezi 20 akiwa mkufunzi wa United,je vimemfikisha pale ambapo alitarajia afike ndani ya msimu wake wa pili akiwa na United?
Inawezekana kwa falsafa zake ni mtu sahihi wa kukujengea timu ya muda mrefu na kukupa mafanikio,je United ilihitaji kujengwa katika misingi mipya hasa baada ya SAF kuuweka msingi mzuri kwa miaka 25 akiwa na timu hiyo. Nafahamu kila mkufunzi ana njia zake katika ufundishaji lakini hili la falsafa na sera mpya za usajili kuondoa kile ambacho kilishajengwa kwa miaka mingi ni sawa na hadhira kukaa bila fanani, hili kwa upeo wangu lilihitaji muendelezo ule ule nje kabisa ya hivyo vitu viwili vilivyoletwa na LVG na muajiri wake Edwoodward.
Wakati LVG akipumua kwa sasa chini ya kivuli cha makinda hawa na bodi ya United ikumbuke kuwa udhamini wa haki za mauzo ya televesheni kuanzia msimu ujao utakuwa ni mnono zaidi na watafiti wa masuala ya uchumi wamesema upo uwezekano wa kuwa na vilabu vyote shiriki vya ligi kuu kutoka England katika 30 bora ya vilabu tajiri duniani. Wakati United wanaendelea na ujenzi wao wa timu kuna vilabu vitaleta kina Payet, Imbula, Shaqiri, Wijnaldum wengine na kuifanya ligi kuwa na ushindani zaidi huku ndoto wanayoiota bodi ya United na mashabiki wake kuwa kama simulizi ya kitabu cha usiku utakapokwisham
Siwaombei mabaya hawa makinda wasifisike pale ambapo wanatarajia tatizo ni hiki kiini macho cha muda mfupi na upenzi unapotia upofu moyo na kusahau nini ambacho LVG amefanya katika kipindi cha miezi 20 iliyopita hapa ndio tatizo langu lilipo.Nilishawaona kina Ravel Morrison, Kiko Macheda na wengineo wengi wakiishia kati kati ya safari pamoja na majina yao kuimbwa sana kipindi chao.. na mimi pia natamani niendelee kuamini kuwa LVG ni mtu sahihi kwa United na kuota hiyo ndoto yake tamu pamoja nae lakini sio katika kipindi hiki ambacho Etienne Capoue yupo pale Vicarage Road huku yeye akiendelea na ujenzi wake wa Manchester United mpya chini ya falsafa ya kidachi.
Z.Bilali
0784111348

No comments