KWA MAANDALIZI HAYA RUVU SHOOTING WAMEDHAMIRIA KURUDI LIGI KUU

Timu ya Soka ya RUVU SHOOTING imezidi kudhihirisha uwezo wake wa kucheza mpira na dhamira yake ya kupanda daraja, kucheza ligi kuu Tanzania Bara msimu wa mwaka 2016/17 kutokana na maandalizi makubwa iliyoyafanya na matokeo mazuri inayoyapata katika mechi za kirafiki inazocheza.




 Timu hiyo inayoongoza ligi daraja la kwanza kundi B, imekuwa kambini kwa muda mrefu ikijiandaa kikamilifu na mzunguko wa pili wa FDL ambapo Jumapili ijayo, Desemba 27, itakuwa katika uwanja wake wa nyumbani Mabatini ikipambana na JKT Mlale, mchezo wake wa kwanza wa mzunguko wa pili wa ligi hiyo.

 Afisa Habari na Uhusiano wa Ruvu Shooting, Masau Bwire alisema kwamba, kikosi cha timu yake kiko vizuri na tayari kwa ajili ya mzunguko wa pili, wa lala salama wa mashindano hayo akitamba kufanya vizuri kutokana na maandalizi makubwa waliyoyafanya kwa kuiandaa vema timu yao.

"Tuna nia na malengo ya dhati kucheza ligi kuu Tanzania bara, ili kufikia malengo hayo tumeiandaa timu yetu kwa ubora na kiwango cha hali ya juu, maandalizi yanayotupatia uhakika wa asilimia zaidi ya 90 kumaliza ligi ya FDL tukiongoza kundi letu B na kutufanya msimu ujao tucheze VPL" alisema Bwire.

Alisema timu yake katika kipindi hiki cha maandalizi imecheza mechi kadhaa za kirafiki na kufanya vizuri ukiwemo mchezo dhidi ya Polisi Dar es salaam uliochezwa juzi Jumapili kwenye uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini, Dar es salaam na kushinda bao 2-1, mchezo wa mwisho wa majaribio kabla ya kuanza mzunguko wa pili wa FDL utachezwa kesho, Jumatano Mabatini dhidi ya KMC ya Dar es salaam.

Msimamo wa FDL, mzunguko wa kwanza kundi B, Ruvu Shooting inaongoza ikiwa na pointi 16, ikifuatiwa na Njombe Mji yenye pointi 13, JKT Mlale ikikamata nafasi ya tatu kwa kuwa na pointi 12, nafasi ya nne ikikaliwa na Kurugenzi  yenye point11, Polisi Morogoro yenye point 10 ikishika nafasi ya tano, Lipuli ipo nafasi ya sita ikiwa na pointi 9, Kimondo Fc  ni ya saba kwa pointi zake 4, mwisho ni Burkinafaso FC yenye pointi 2.

No comments

Powered by Blogger.