NEYMAR PIGA GOTI, KAZI NI UNAFIKI TU



Na Nicasius N Agwanda ( Nicasius Coutinho Suso)

Katika moja ya makala zangu, niliwahi kuandika hakuna lililo sawa katika dunia hii isiyo sawa. Niliandika  nikilenga hasa juu ya uwezo wa Eden Hazard pia nikimhusisha Angel Di Maria na  kwanini pengine wanaweza kuja kuwa mchezaji bora wasiokuwa na ushindi wa kiuchezaji nikizungumzia tuzo kubwa za heshima duniani. Ilikuwa vyema sana kumuona Hazard akishinda tuzo ya mchezaji bora wa ligi kuu ya Uingereza msimu uliopita lakini bado nasimama kuwa ingekuwa rahisi zaidi kumpa Sanchez tuzo ile kama tu ule ungekuwa msimu wake wa pili katika klabu ya Arsenal bahati mbaya alikuwa na msimu wa kwanza tu. Dunia imebadilika sana, dunia imehama kutoka kwenye maisha ya mchezaji bora kutajwa kwa burudani na mchango tofauti tofauti ndani ya uwanja na nini umeshinda kama timu mpaka kwenda kwenye wingi wa magoli yako mguuni. Hapa ndipo Hazard na Di Maria wanashindwa, hapa ndipo Sanchez anaonekana bora maradufu katika klabu ya Arsenal na ligi kuu ya Uingereza, na hapa ndipo palipokuwa pameficha maovu yote ya Suarez na mashabiki kuona kama ni malaika aliyekuwa katika mfumo wa kibinadamu.

Dunia kamwe haikomi na haitokoma kuzunguka katika muhimili wake ikimaanisha kuwa siku hazigandi, maisha yamemchukua Van Persie, yakamsomba Falcao, yalikwishamzika Torres na sasa yanaonekana kuanza kuwachoka Messi na Ronaldo. Bahati mbaya ni kuwa hawa wanabaki kuwa wa kipekee sana, wana vipaji na hawajimalizi kianasa. Wakati Ronaldo akiwa mtu wa kujiremba na mitoko lakini muda mwingi wa maisha yake unamalizikia katika chumba cha mazoezi na uwanjani. Yule mtu mfupi ana kipaji asilia, yeye zile sindano za kumkuza pengine zilikuwa na virutubisho vya ziada ambavyo vimemfanya awe hivi alivyo. Lakini pamoja na yote hayo swali linabaki baada ya hawa anafuata nani? Dunia itamkumbatia yupi na ni kwa namna gani anastahiki hiyo heshima? Umemuona Neymar, pengine namna yake ya maisha inaweza kuwachukiza wengi, lakini ndivyo wabrazil walivyo, wao maisha bila kioo cha kujitizama ukishakuwa maaarufu ni kutokutimiza wajibu.

Lakini ulimwengu wa sasa hivi unawahitaji wa aina yake, wale wanaojua upande ambao goli limelalia hata kama wakivikwa kiziba uso. Tatizo kubwa ambalo anakutana nalo Neymar ambalo kimsingi limemuathiri pia Gareth Bale katika vilabu vyao ni uwepo wa wafalme kabla yao. Binadamu  ambao kila jicho la mpenzi wa soka limekuwa likiwatizama kwa umakini wa hali ya juu, watu ambao wameigawa dunia pande mbili na kila mmoja akachukua wake. Kule katika timu ya taifa Neymar hakuwa na shida, anafanya anavyotaka na anafunga anavyojisikia. Katika miaka isiyozidi mitatu atakuwa mfungaji bora wa muda wote wa nchi yake kama akiendelea na kasi hii. Swali lilikuwa limebaki moja tu, ni lini Neymar wa Brazil atavaa jezi ya Barcelona? Maana kwa kipindi chote hiki walikuwepo Neymar wawili uwanjani, Yule wa Rio De Janeiro na Yule wa kule Catalan. Msimu uliomalizika ndipo ambapo Neymar alianza kuonyesha ukomavu hasa, kitendo cha kuikubali khali na kuyaacha maneno ya Pele kuwa ni Mchezaji bora anayefuata  ilimjenga na alifunga sana, kuwa mfungaji bora wa UEFA sio jambo dogo, na pamoja na kutokumulikwa sana lakini huyu aliamua maisha ya Barcelona katika hatua za mwisho za Uefa.

Bahati nzuri huja na ubaya wake, ili wewe ufanikiwe inabidi mwingine ayalipie mafanikio yako yaani ili nyota yako ing’ae basi kuna nyingine itakayopaswa kufifia japo kwa muda. Neymar alihitaji nafasi tu kucheza kwa uhuru ili aondoe ule wasiwasi juu yake. Alihitaji siku ifike mapema aweze kujaribu kuiweka Barcelona mabegani na kuishi maisha yale ya Santos katika timu ya taifa Brazil. Soka ni mchezo ambao watu wanataka ubora wa sehemu moja uhamishie kwingine, na kwa wachezaji kariba ya Neymar au Bale hawakuhitaji kucheza sana kwenye vivuli vingine kwa muda mrefu, hii ndio sababu iliyoficha uwezo wa Sanchez kwa kipinid kirefu, hiki ndicho chanzo cha ugumu wa maisha ya Zlatan pale Barcelona na huku ndiko kulimzamisha David Villa, ndio maana Benzema na James Rodriguez hawapati heshima wanayostahiki kule Bernabeu. Nilikuwa natizama namna ambavyo Neymar atapokea taarifa za majeraha ya Messi, nilijua kuna mambo mawili. Mosi ni kuumia machoni na uchungu moyoni kutokana na Messi kuwa swahiba wake mkubwa sana na wa karibu, lakini pili ilikuwa furaha miguuni kwake.


Ndio miguu yake ilihitaji faraja maana inafanya kazi na kazi haina rafiki wa karibu na wala haina mapenzi ya dhati, katika hili kila binadamu huwa mnafki. Kila mmoja anatamani kuweka maisha yake mbele na kufanya kazi anayotakiwa kwa umakini mkubwa. Kama ni beki kaba sana, kama ni kipa daka kwa umaridadi na kama ni mfungaji funga bila kusita. Kule Brazil mipira yote inamtizama yeye Neymar  yupo wapi, huku Barcelona mipira ilibidi iwafikie wawili kabla yake na wahakikishe Yule mmoja anaipata mingi haswa. Nilikuwa natizama michezo baada ya majeraha ya Messi huku Suarez akiwa anahaha kurudisha fomu yake ya msimu uliopita, Neymar anafanya majukumu kwa ukomavu. Amekuwa baba mlezi wa timu, amekuwa mshambuliaji korofi (aggressive) na amekuwa msaada mkubwa. Anafunga akitaka na anasaidia upatikanaji wa magoli. Huyu ndiye Neymar ambaye Santos walimwekea dau la kumuuza kwa Euro 25m akiwa bado hajaanza kucheza timu ya wakubwa, huyu ndiye Neymar ambae Barcelona ilibidi waingie kwenye skendo ya matumizi mabaya ya pesa kumpata. Huyu ndiye Neymar aliyekuwa tofauti na Hazard. Kwa sasa anaongoza orodha ya wafungaji La Liga, bahati nzuri ameshaijua ladha ya makombe, akiendelea hivi Ballon D’or ipo nyuma ya mgongo wake inamfuata lakini kikubwa apige goti Majeruhi yawe sehemu ya maisha ya Messi msimu huu, ili akirejea amkute akiwa kaishajiamini na timu amejikabidhi. Ndio kazi ni unafki na bahati nzuri ana muonekano wa kibiashara pengine tofauti na mchezaji mwingine yoyote, atatangazwa tu na wala usimchukie.

Ahsanteni.


Insta @Nicas.coutinho

No comments

Powered by Blogger.