KOCHA WA YANGA AJIPANGA NA MECHI ZA UGENINI
Kocha Mkuu wa Yanga, Hans Pluijm ametamba kuandaa kutumia mbinu maalum zitakazoiwezesha timu yake kuvuna pointi kwenye viwanja vya ugenini jambo litakaloiweka kwenye mazingira mazuri ya kutetea Ubingwa wa Ligi Kuu.
Yanga inayoongoza ligi ikiwa na pointi 19 baada ya kucheza michezo saba, mpaka sasa imecheza mechi mbili ugenini ambazo kati ya hizo ni moja tu iliyocheza nje ya jiji la Dar es Salaam, ambapo ilikutana na Mtibwa Sugar kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro ikishinda kwa mabao 2-0.
Timu hiyo sasa inakabiliwa na mechi tatu mfululizo kwenye viwanja vya ugenini dhidi ya timu za Mwadui, Kagera Sugar na Mgambo JKT ambazo zinatajwa na wadau wengi wa soka kuwa pengine zinaweza kutoa taswira ya mwenendo wa timu hiyo kwenye Ligi Kuu msimu huu.
Pluijm alisema kuwa ingawa anazipa uzito sawa timu zote zinazoshiriki Ligi Kuu, hali ya viwanja vya ugenini vinamfanya aandae mbinu maalumu za kiuchezaji kwa kikosi chake ili waweze kuibuka na ushindi utakaozidi kuwaweka kwenye nafasi nzuri ya kutetea taji lao.
"Unapokuwa kwenye viwanja vya ugenini ni tofauti kabisa na kucheza kwenye uwanja wa Taifa. Viwanja vingi huko havina sehemu nzuri ya kuchezea jambo ambalo linaweza kuathiri kiwango cha timu na wachezaji. Kikubwa ninachokifanya ni kuwaandaa wachezaji wangu na kuangalia ni kwa namna gani tunaweza kumudu mazingira ya viwanja hivyo na kuweza kupata ushindi utakaozidi kutuweka mahala pazuri," alisema Pluijm.
Pluijm aliongeza kuwa Yanga ina wachezaji wazuri ambao wanaweza kuamua matokeo katika uwanja wowote ule kama ambavyo waliweza kufanya hivyo kwenye uwanja wa Jamhuri dhidi ya Mtibwa Sugar.
No comments