STARS KUWASILI NCHINI LEO KUWAVAA NIGERIA JUMAMOSI
Baada ya kuwa na kambi ya takribani wiki moja nchini Uturuki, timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro leo usiku inarejea nyumbani tayari kwa maandalizi ya mwisho kabla ya mchezo wake dhidi ya Nigeria Septemba 05, 2015 siku ya Jumamosi.
Kwa mujibu wa Kocha Mkuu wa Stars Charles Mkwasa timu yake imepata nafasi nzuri ya kujiandaa na mchezo huo wa Jumamosi, kwani vijana wamepata kufanya mazoezi katika mazingira mazuri yenye utulivu na kuonyesha umakini mkubwa katika mafunzo waliyokuwa wakielekezwa.
Mara baada ya kuwasili jijini Dar es slaam leo usiku, Stars itaingia moja kwa moja kambini ambapo wachezaji wanaocheza soka nje ya nchi, Mrisho Ngasa, Thomas Ulimwengu na Mbwana Samata wataungana na timu kasha jumatano kufanya maozezi jioni katika uwanja wa Taifa.
Msafara wa Stars unaongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Ahmed Mgoyi unatarajiwa kuondoka Uwanja wa Ndege wa Istanbul saa 1 usiku na kutua Uwanja wa JK Nyerere jijini Dar es salaam saa 9 kasoro kwa usairi wa Shirika la Ndege la Uturuki (Turkish Airlines).
Stars iliweka kambi nchini Uturuki kujiandaa na mchezo dhidi ya Nigeria wa kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa Afrika (AFCON) mwaka 2017.
No comments