VILABU VYATAKIWA KUWASILISHA NAKALA 3 ZA MIKATABA TFF
Klabu za Ligi Kuu ya Vodacom
(VPL) zinatakiwa kuwasilisha mikataba ya wachezaji wake- nakala tatu kwa kila
mchezaji kwa ajili ya kuidhinishwa na TFF, kama ilivyoelekezwa katika Kanuni ya
69(1) na (8).
Baada ya mikataba hiyo kuidhinishwa ikiwa ni pamoja na
kulipiwa ada ya sh. 50,000 kwa kila mmoja, nakala moja itakuwa ya klabu,
nyingine ya mchezaji na moja itabaki TFF ili linapotokea tatizo la kimkataba
uamuzi ufanywe na vyombo husika mara moja.
Pia klabu ya VPL inatakiwa kuwasilisha TFF orodha ya
benchi lake la ufundi, mikataba ya maofisa wa benchi husika pamoja na nakala za
vyeti vyao. Kwa mujibu wa Kanuni ya 72 (3), Kocha Mkuu anatakiwa kuwa na Leseni
ya CAF isiyopungua ngazi B wakati Kocha Msaidizi anatakiwa kuwa na Leseni ya
CAF isiyopungua ngazi C.
Kwa upande wa timu za Ligi Daraja la Kwanza (FDL), Kocha
Mkuu anatakiwa kuwa na Leseni ya CAF isiyopungua ngazi C wakati msaidizi
anatakiwa kuwa na cheti kisichopungua ngazi ya Kati (Intermediate).
Hakuna kocha asiyekidhi makatwa hayo ya kikanuni
atakayeruhusiwa kuongoza timu yoyote kwenye mechi za ligi hizo mbili. Pia
viongozi wa klabu wasiozingatia maelekezo haya, wanakumbushwa kuwa wanakwenda
kinyume cha kanuni.
No comments