STARS YAENDELEA KUJIFUA UTURUKI

Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) ipo nchini Uturuki, imeendelea na mazoezi jana asubuhi katika viwanja viliyopo kwenye viunga vya hoteli ya Green Park – Kartepe.
Mara baada ya kuwasili jumatatu jioni katika eneo la Kartepe, timu ilifanya mazoezi jioni kwa takribani saa moja na nusu, kuanzia saa 1 jioni mpaka mida ya saa 3 kasoro usiku, ambapo leo na kesho itafanya mazoezi asubuhi na jioni.
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles Mkwasa amesema huduma na vifaa vilivyopo katika hoteli waliyofikia (viwanja, gym) wanavyotumia kwa ajili ya mazoezi ni vizuri, hivyo ratiba yake ya mazoezi inakwenda kama alivyopanga katika maandalizi ya wiki moja ya kuajiandaa na mchezo dhidi ya Nigeria.
Taifa Stars inatarajiwa kucheza mchezo wa kirafiki wa mazoezi na timu ya Taifa ya Libya siku ya ijumaa, ambapo kocha Mkwasa atatumia nafasi hiyo kupima kikosi chake baada ya kuwa wamefanya mazoezi kwa siku nne nchini Uturuki.


Kikosi cha wachezaji 21 chini ya kocha mkuu Charles Mkwasa, na msaidizi wake Hemed Morocco, kocha wa makipa Peter Manyika na mshauri wa benchi la ufundi Abdallah Kibadeni wanaendelea kuwanoa vijana vilivyo kwa ajili ya mchezo wa mwezi Septemba dhidi ya Nigeria.


No comments

Powered by Blogger.