ADIOS PIRLO, UKISAHAU TUTAPIGA WALAU PICHA.
Jibu sahihi hutokana na swali sahihi lakini nalo swali linatakiwa litokane na mtu sahihi katika mlengo sahihi. Ni kama ambavyo huwezi kupata jawabu la sheria kutoka kwa mkandarasi au ubora wa muziki kutoka kwa kiziwi. Lakini yote haya huambatana na jambo moja tu usahihi. Macho yangu yamewahi kushuhudia vitu vingi vilivyo vya kweli, vizuri na kuwa Shahidi wa vilivyo bora pia. Macho yangu hayakuwahi kujutia kutizama pasi za Xavi Hernandez , kuona magoli ya Steven Gerrard, kufurahia madoido ya Ronaldinho Gaucho au kuwa shahidi wa vionjo vya Zinedine Zidane zizou. Lakini niliyanyima uondo mmoja tu, nao ni kupanua mboni kwa ajili ya Andre Pirlo. Sio mimi tu hata ulimwengu uliruhusu Muda mdogo sana wa kumtizama huyu. Wachambuzi wa mambo walifunika sana uwezo wake huyu. Na mwisho dunia hii isiyo sawa ikapatwa na upofu juu ya uwezo wake huyu binadamu. Wanasaikolojia wanakwambia hakuna kinachouma kama kuelezwa ukweli usiotaka kuusikia.
Ni katika dunia hii ambayo Pogba ameimbwa kuliko Andre Pirlo pale Juventus, ni katika dunia hii ambayo watu waliumizwa na Ricardo Kaka kupotea mapema kuliko Pirlo kutokuwepo walau katika kikosi bora cha mwaka mfululizo. Ni katika dunia hii ambayo Pirlo atastaafu huku jina la Arturo Vidal ni maarufu kuliko lake. Yote haya yanaambatana na neno moja tu la kiingereza UNDERRATED. Khali ya kutopewa heshima unayostahiki. Unataka nini kutoka kwa kiungo wa kariba ya juu ukikose kwa Pirlo. Mungu hakumpa kasi lakini alimpa akili ya kufanya kasi ionekane haina maana katika soka. Na mwisho akafanya kazi iliyowashinda wengi. Kazi iliyomfanya Gerrard akateleza, kazi ambayo Zidane asingethubutu kuifanya, na kazi ambayo Ronaldinho hajawahi kuwaza rohoni kuifanya. Inaitwa REJESTA kwa Kiitaliano. Maana yake unamchukua kiungo mshambuliaji kwa kiingereza Central Attacking Midfielder (Trequartista kwa Kiitaliano) unambadili kuja kucheza mbele ya mabeki Muda mwingi ndio anakuwa ndio mchezaji huru uwanjani lakini anakuwa amiri jeshi kwa maana ya kuamua timu icheze vipi.
Bahati mbaya ambayo Pirlo amewahi kukutana nayo ni kutokua na sura ya matangazo na ukimya wake kiuchezaji. Mara nyingi maishani mwake ameambatana na watu wa kariba hii. Kipindi anaishi na akina Zidane, Ronaldinho Kisha Kaka wote walikuwa na tabia hii ambayo huyu aliikosa. Na wakati wale Waingereza wakimuimba Lampard lakini hakuwahi kuwa na akili hii ya huyu mtu. Lakini ni huyu huyu ambaye katika kikosi bora cha FIFA cha mwaka ametokea mara chache kuliko Xabi Alonso. Kuna wakati wanazaliwa wachezaji wengi wenye tabia hii, tabia ya kutokuimbwa sana. Ndugu yake huyu anaitwa Bastian Schweinstiger. Wakati Buffon akiamini hajazaliwa mchezaji mwenye akili katika Taifa la Italia kama Pirlo baada ya Roberto Baggio, wakati macho yangu yakishuhudia mchezaji mtimilifu zaidi katika uwezo wa pasi, dunia tuliamua kwa makusudi kuamini hakuna kiungo kama Sneijder, Xavi na Iniesta.
Walau Kuna wakati unafika hata yule uliyemuamini anakuonyesha Kuna mwingine ulitakiwa kumuimba pia. Baada ya kosa kubwa la dunia, walau macho ya Xavi yalionyesha hata yeye kakutana na alichokihusudu. Wakati wa fainali ya Uefa champions League pale Berlin, ukaribu wao ungekupa jibu zaidi. Macho yao wote wawili yalionekana kukubaliana katika jibu moja tu, kuwa vilivyo bora vilikaa mahala pamoja. Walau kwa mara ya kwanza kamera zilizungumza ukweli lakini kupitia katika macho ya Xavi. Hakuna namna nyingine, dunia ilimweka kando na yeye atamaliza akiwa kando huko. Ipo siku mwanae atasoma, maandishi yatamwonesha kuwa baba yake hakuwahi kufika uwezo wa Gerrard, lakini mikanda ya video itatamka tofauti. Ni kama ambavyo baada ya leo wengi kusoma hapa tutatamani kumwomba Pirlo msamaha lakini aibu itatujaa machoni. Tunasubiri aweze kusahau ndio tuseme, hata mimi nipo hapo. Nasikia yupo anajiandaa na safari ya Marekani, nachukua fursa hii kumuaga tu. ADIOS PIRLO, ndio hivyo naona aibu kama wanadamu wengine watakavyokuonea aibu kuanzia leo si unajua Kuna wale walioamini katika Fabregas, na wale walioamini katika Carrick, Modric bahati mbaya Kuna na hawa wameamua kuamini katika Henderson, lakini nasubiri ukishasahau nitakutafuta tupige picha.
Ahsanteni. By Nicasius Nicholaus Agwanda ( Nicasius Coutinho Suso).
No comments