SAKATA LA SINGANO NA SIMBA NI ALAMA KUWA SOKA LETU LINAENDESHWA KIHUNI


Wakati suala la mchezaji wa Simba Ramadhani Singano likiwa linapamba moto katika vituo mbalimbali vya habari nchini Tanzania,barani Ulaya ule wakati wa kutumia pesa kwa vilabu katika bara hilo umefika na kuwanufaisha watu kama kina Jorge Mendes wanaojua maana sahihi ya kitu kinachoitwa kalamu..

Tukiwa bado tupo nyuma katika usomaji wa alama zetu za nyakati wenzetu huwa wanapanga na kupangua kabla hawajachelea na kumkuta mwana si wa kwao..kuna vitu viwili ambavyo wachezaji wa Tanzania kila kukicha na uchwao hawapigi hatua wakati wanasaini mikataba yao na suala la muda hawalizingatii kabisa hawawazi kesho yao itakuaje atakapoachwa na Simba, Azam au Yanga au atakapotakiwa na timu kutoka nje ya Tanzania itakuaje tungepata nafasi walau ya kuona wanachokiwaza wakiwa wamezungukwa na viongozi wa hivi vilabu vikubwa hapa nchini wakati wa usajili labda tusingewalaumu wachezaji husika,vilabu na hata TFF.

Suala la mkataba wa mchezaji Ramadhan Singano limekua likitembea kwa kila upande kumrushia mwenzie mpira ili aonekane ana makosa mchezaji anadai mkataba wake mwisho 2015 wakati klabu inasema mwisho 2016 na mbaya zaidi wote wana vithibitisho na hapo ndipo uozo wa mikataba ya wachezaji wetu unapoanzia kesi kama hizi zipo nyingi tu hili la Singano ni mfano wa jinsi soka letu linavyoendeshwa kihuni

Mchezaji anafikiria zaidi pesa wakati anasaini kuliko yale maandishi yaliyopo kwenye karatasi nyeupe ambayo yana umuhimu mkubwa hapo ndipo maana ya kuwa na wakala anayekusimamia shughuli zako za nje ya uwanja inapoonekana na wachezaji wetu wengi hawana ule utambuzi kwamba ile ni kazi na cha kusikitisha utakuja akiwa umri umeshakwenda na kichwani mwake atabaki na historia ya kumnyanyasa Yondani au Mbonde pale uwanja wa taifa kizazi chake hakitajivunia kutajwa jina lake na kina Martin Tyler au John Champion akiwa anacheza katika nyasi za Anfield.

Ufike wakati kila mchezaji awe na mtu wa kumsimamia na kumchambulia vifungu vya mkataba wake ulivyo sio upigiwe simu tu huyo moja kwa moja unaenda kusaini tu hujui hata nini kimeandikwa na hata hauringi kuonesha ile thamani yako,mchezaji mzuri ni bidhaa adhimu sana ambayo kama haikuchungwa vizuri hupotea kama almasi kwenye mchanga wa jangwani..kutokujithamini kwa wachezaji na vipaji walivyo navyo kunasikitisha na ile kujiona ni watu wa kawaida vilabu na vyenyewe vinawachukulia hivyo hivyo na kuwasainisha mikataba ya hovyo.

Ndio hawa hawa wachezaji ambao wana umoja wao wa wanachama ule name wengine sidhani hata kama wanaujua hivi wameshindwa kabisa kuwa na watu maalumu wa kuwasomea mikataba kwanini wasiajiri wanasheria kadhaa kupitia ule umoja wao wawe wanawalipa kitu ambacho kinawezekana kabisa na hawawezi kushindwa kama watakua na ushirikiano na mshikamano ili wasimamiwe lakini la kuhuzunisha bado mpaka leo katika soka la kisasa wanachukua ndugu zao wasio na utaalamu wowote kuhusiana na masuala ya mikataba kupata unafuu.

Binafsi suala la Singano silifurahii kwanza linamuathiri kisaikilojia kama mchezaji na mbaya zaidi anaongea na vyombo vya habari mno na kuukaribisha msukumo usio na tija kazi ambayo wakala alitakiwa awepo kuifanya inafanywa na mchezaji husika. Inaumiza sana na kusikitisha lini na sisi wachezaji wetu watakuwa na mikataba bora sio bora mikataba ili wafikirie zaidi maendeleo ya soka lao.

~ Na Bilal (Wapenda Soka)

No comments

Powered by Blogger.