STARS YAENDELEA KUJIFUA SAUZI


Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) imeendelea na mazoezi katika uwanja wa Olympia Park kujiandaa na mchezo wa fungua dimba dhidi ya timu ya Taifa ya Swaziland.

Kocha mkuu wa timu ya Taifa Stars Mart Nooij amesema vijana wake wanaendelea vizuri na mazoezi, ikiwa leo ni siku ya pili kufanya mazoezi baada ya kufanya mazoezi ya kwanza jana jioni.

Nooii amesema japokuwa kuna hali ya hewa ya baridi katika mji wa Rustenburg, wachezaji wake wameanza kuizoea na kusema kwa kuwa bado kuna zaidi ya masaa 72 kabla ya mchezo wa awali watakua wameshaizoea hali ya hewa.

Kuhusu uwanja wa mazoezi, kocha Nooij amesema hali ya uwanja ni nzuri, uwanja una nyasi nzuri hali inayopelekea kikosi chake kufanya mazoezi katika mazingira mazuri.

Akiongelea mchezo wake wa kwanza wa ufunguzi dhidi ya timu ya Taifa ya Swaziland utakaochezwa siku ya jumatatu, amesema anawajua Swaziland ni timu nzuri, mara ya mwisho katika mchezo wa kirafiki walitoka nao sare, hivyo anawaanda vijana wake kupata ushindi katika mchezo huo.

Kikosi cha Swaziland kina wachezaji mchanganyiko wakiwemo wanaocheza ligi yao ya nyumbani na baadhi wanaocheza soka la kulipwa nchini Afrika Kusini.

Taifa Stars itacheza mchezo wa kwanza dhidi ya Swaziland katika Uwanja wa Olympia Park siku ya jumatatu saa 1.30 usiku kwa saa za huku, sawa na saa 2.30 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.


IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)



No comments

Powered by Blogger.