KUELEKEA FAINALI, MAMBO KUMI NILIYOJIFUNZA BAADA YA NUSU FAINALI UEFA CHAMPIONS LEAGUE.
1. Hakuna ukweli unaouma kama ule wa Gareth Bale kutua kwa mpinzani wako msimu ujao. Lakini ndio ukweli wenyewe, Pamoja na uzuri wake kiuchezaji lakini Gareth Bale anabaki Kuwa weak link (sehemu Isiyo na nguvu) katika kikosi cha Madrid. Hii inaweza Kuwa inaambatana na tatizo La kisaikolojia lakini pia hili ni tatizo kwa wachezaji wanaotoka wakiwa tegemezi zaidi katika vilabu vyao, kuja Kuwa chini ya wafalme wengine. Unaweza kutabiri Kuwa Perez atamnufaisha mtu na Bale na pia atamdhoofisha mtu kwa kuchukua mbadala wa Bale. Namuona Hazard kwa mbali, maana alichokuwa anasubiria amekipata (taji la ligi kuu kapata) hilo la ulaya unalishinda kwingine kokote.
2. Moja ya makosa makubwa ambayo Guardiola amewahi kuyafanya basi ni lile alilofanya dakika 15 Za mwisho Camp Nou. Kwa kocha wa kariba yake alitakiwa kujua Barcelona waliamua kususia mpira ili wamtafute kwenye counter attacks au kwenye makosa binafsi maana alishawapatia. Na namna pekee ingepatikana kwa yeye kama Bayern wangeshambulia sana hivyo kupunguza watu nyuma, unapokuwa unacheza na Messi, Suarez na Neymar unahitaji zaidi kujilinda ugenini na kuhimili presha. Guardiola aliwanyima walichotaka Barcelona dakika 75 halafu akawapa kwa dakika 15. Sidhani kama aliwahi kukosea tena hivi. Sare kwake ilikuwa safari nzuri.
3. Makala iliyopita niliwapa Juventus Jina la UNDERDOG SYDROME. wanaishi kama wanyonge lakini tutawakumbuka Berlin. Na hawajaniangusha, huwezi Kuwa na Vidal, Pirlo, Tevez, Marchisio, Pogba ukaita hii timu ndogo. Ila wanatumia vizuri uhusika wa Kuwa Underdogs. Narudia kusema kama makala iliyopita kwa mwendo huu wa kobe alihitimisha safari ndefu na ngumu,tusubiri maana Kuona ni kuamini.
4. Unahitaji kujua mwanadamu asiye na amani Zaidi kwa sasa duniani? Si mwingine bali ni Chiellini na Evra. Waswahili siku hizi wanasema usiyempenda kaja. Fainali itakuwa tamu hapa, hawa wawili dhidi ya Luis Suarez. Kwenye maisha yake ya soka Luis Suarez amekuwa anafanya sana Donkey Jobs(kazi Za punda). Kwa asilimia 25 mechi Ile itaamuliwa na kichwa chake . Akitulia ataweza na Barcelona hawatozuilika,asipotulia ameiua kama ilivyotokea dhidi ya Munich alipotolewa.
5. Kuna makocha watatu waongo Zaidi duniani. Yupo Wenger anaeamini Giroud (Pamoja na fomu yake) Kuwa atampa medali ya Fedha (kombe la ligi au ulaya), mwingine ni Fillipo Inzaghi anayeamini Essien na Muntari wanaweza kuirudishia Ac Milan makali na mwingine ni Carlos Dunga anayetuaminisha Kuwa Felipe Luis ni bora kuliko Marcelo. Yule Marcelo anaweza Kuwa ndio beki mbunifu Zaidi wa kushoto kutokea kwa miaka ya karibuni. Huyu huwa silaha kubwa ya Playmaking (kutengeneza mashambulizi) kuliko hata viungo hata dhidi ya Juventus alikuwa hatari kuliko Bale, Ronaldo, Benzema.
6. Silaha kubwa wanayoitumia Juventus na wengi bila kujua basi ni uwepo wa Alvaro Morata. Hazungumzwi sana lakini ndiye anayefanya Tevez azunguke vile, Vidal awe huru vile na mabeki wa timu pinzani wasitulie. Uwezo wake wa kuja nyuma kupokea mipira ndio unaofanya Juventus iwe na mlinganyo na uwiano mzuri wa kiuchezaji. Bahati mbaya hatuna box to goal striker ila hili Jina lingemfaa. Tuombe Mungu kiwe kipaji kingine ambacho hakitapotea
7. Tofauti aliyoiweka Massimiliano Allegri kwa Juventus, ambayo Conte alikosa ni Ile ya YATIMA HADEKI. Kila mchezaji wa Juventus ni willing runner (atakimbia panapobidi), wanamlinda Pirlo inavyostahiki, sababu kuu ni Kuwa hawana namna nyingine ya kushinda zaidi ya kucheza kwa roho ya chui. Kwenye soka wao ni yatima tu, baba yao Serie A alishajifia mapema. Hii inaweza Kuwa silaha kubwa kuliko chochote. Uwezo wa kucheza Tisa nyuma ya mpira na kufanya counter attacks kali ni jambo ambalo wamelifanya vyema kuliko timu yoyote mpaka sasa. Kuna namna mbili Za kuizuia Barcelona hii, ya kwanza ni kuwafunga magoli mengi ili wakikufunga isiwe shida (anayeweza kujaribu hapa ni Madrid tu), na nyingine ni kuwakimbiza sana na mipira miguuni wasipate mwanya wa kutulia, ukiwapokonya unapiga counter attacks. (mwenye hii silaha ni Juventus pekee.) tatizo linabaki Kuwa moja daima MSN. Ingawa dawa moja ishaanza kuonekana, mzuie Suarez ili wengine wasicheze maana huyu ndo mwenye Pete ya ndoa kule mbele (anawahusanisha Messi na Neymar)
8. Laiti kama Kamera Za Uefa na Fifa zingekuwa zinamulika vyema, Chiellini anabaki Kuwa moja ya mabeki bora zaidi kuwahi kuukanyaga huu Ulimwengu. Bahati mbaya alizaliwa siku mbaya. Wakati anakua walikuwepo akina Nesta, Maldini alipokomaa wakaibuka akina Vidic na wakati anamalizia wameibuka akina Ramos ambao pamoja na vipaji vyao uhuni na uwezo wa kuamua matokeo kwa magoli yao vinazivutia zaidi kamera.
9. Papa hawezi kuiongoza Urusi au Korea Kaskazini. Atazuia kutengenezwa kwa silaha nzito na kuhubiri amani. Ni kama ambavyo siku zote niliamini Pep Guardiola hakuwa mtu sahihi wa kwenda Bayern Munich. Sio kwa sababu sio mzuri au hasingeipa mafanikio. Ni kwa sababu hii tu Kuwa kwa Muller atamtaka Gotze, kwa Schweinstiger atamtaka Alcantara, kwa Martinez atamweka Lahm. Heynckes Pamoja na udhaifu wa Barcelona aliwapiga kwa sababu alienda ofisini na Caterpillar na sio Benz. Ule mpira laini ni wa Hispania, hata huko aliko Adolf Hitler anaamini Guardiola anaharibu tamaduni Za wajerumani.
10. David De Gea, Thibaut Courtouis, Simon Mignolet, Claudio Bravo.. Hapana hata Manuel Neuer bado ana safari ndefu ya kufika kwa Iker Casillas na Gigi Buffon. Kwa kifupi duniani ilishuhudia makipa bora zaidi kutokea wakiwa pande mbili tofauti wakicheza na mvi kichwani. Siku nikipata mwanangu nitamueleza Kuwa mwaka 2015 walikaa langoni makipa wawili waliocheza kwa kiwango cha juu kwa miaka 15 na Zaidi. Ni nyani pekee anayeweza kukwepa mishale mingi ukiwaondoa hawa wawili.
NB:
Kuna tofauti moja kubwa ya Msingi Kati ya Lionel Messi na Cristiano Ronaldo Pamoja na ufanano wao mwingi kuanzia uwezo wao wa kufunga, Kuwa wao ndo wachezaji bora Zaidi kwa sasa, na wote Kuwa wafalme vilabuni kwao. Kinachowatofautisha sana kwa sasa ni ule uwezo wa kubaki mchezoni. Hapa ndipo Messi anakuwa wa tofauti zaidi duniani, wakati timu ikiwa imefungwa mara nyingi unakuwa na uhakika Ronaldo atatoka mchezoni, anaathirika na mifadhaiko kuliko mwenzake huyu, zile dakika kuanzia 70 basi Ronaldo atakua mchezoni kwa asilimia 20 na 80 hayupo. Kwa lugha nyepesi Kuna wakati mwingi utamkosa Ronaldo pale unapomhitaji zaidi kuliko inavyotokea kwa Lionel Messi.
Ahsanteni. By Nicasius Coutinho Suso
No comments