MSIMU MPYA CAF & VPL, YANGA WEKENI PICHA UKUTANI



Hakuna uchawi katika maendeleo Zaidi ya kitu kinaitwa maandalizi. Hili ndilo somo rahisi ambalo waafrika kwa ujumla limetushinda. Nchi hazijajipanga kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia, hazijandaa mazingira sahihi ya kukomaza uchumi wao, vyama vya siasa havina maandalizi sahihi ya kujikwamua kutoka katika matatizo yao, mwisho na mafanikio katika sekta pendwa ya michezo yanakwama hapa, hatutaki kujiandaa, hatuwazi kesho bali tunaitizama jioni ambayo katika khali ya kawaida ishawadia. Ni kipindi hiki ambacho hatujui namna ya kuifunga Nigeria iliyovunjika uti wa mgongo na kuitatiza Misri inayotembelea mguu mmoja. Swali ni je hatuwezi? Jibu ni rahisi tu hatujaamua kufanya hivyo au hatujaamua kuweza.

Akili zetu zinawaza kumshinda jirani mwenye ukoma kuliko kupigwa na baunsa mwenye afya. Uliwaona yanga msimu uliomalizika? Walikuwa wanatakata hasa, walifunga walivyotaka, walikimbia na mpira, wakapiga pasi maridadi kisha wakaamua kukaba kwa falsafa ambayo moja kwa moja ungeamini kuwa walikuwa wameyafuata yale mafunzo yanayotakiwa na mwalimu.

Ilikuwa yanga tofauti na tuliyoishuhudia katika miaka ya karibuni. Lakini ukitaka kujiuliza kuhusu msimu mpya lazima uwaze, je ni kweli wamejipanga, je wanajua wanatakiwa kushiriki mashindano ya kimataifa ambayo ni magumu kuliko haya waliyoyamaliza, je wanatambua kuwa wao ni mabingwa wa bara au wanatambua kuwa wameshinda ubingwa tu (kuna tofauti kati ya kuwa bingwa na kushinda ubingwa)?  Kuna tatizo moja linalovitafuna vilabu vyetu kwa kiasi kikubwa, limekuwa gonjwa na linaonekana kukosa dawa, nalo ni Usajili. Huwa Napata shaka kama hivi vilabu vina kitu kinaitwa SCOUTING. Ni miaka kadhaa sasa yanga hawajapata aliye bora kuliko au anayemfikia Niyonzima, na imepita misimu sasa hajapatikana mwenye kipaji cha Okwi Simba. Lakini unajiuliza ni kweli hawapo watu wa namna hii, je hakuna walio bora kuliko hawa Afrika mashariki na kati, je ni kweli hakuna mtu wa kuja kuongeza ubora kama wa Kipre Chetche pale Azam. Jibu linakuja rahisi tu kuwa hatupo makini katika maandalizi.

Hatujui lini tunahitaji hiki, kwanini tunakihitaji na vipi tutakipata. Huwezi kuishi katika mtumbwi daima, utahitaji nyumba au makazi, huwezi kula nyasi siku zote unahitaji chakula stahiki kwa afya. Hivi vyote ni kama kuna dharula, au pale inapobidi ndipo utaishi katika mtumbwi na utakula nyasi, lakini sio vya kutegemea. Lakini sisi dharula ndio tunayoitegemea Zaidi, hatujawahi kuwa na kipindi ambacho tuna mizizi imara kabisa inayoweza kusimamisha ama kushikilia mti. Unamsajili Sserrunkuma kisha unamtema ndani ya msimu mmoja, unamsajili Jaja unamuacha ndani ya miezi kadhaa, unamkimbilia Umony kisha hujui matumizi yake unaamua kumuacha kisha unawalipa pesa ambayo ungewakuza vyema Makapu, Hajib na Kelvin Friday. Kwanini Okwi asijihisi mfalme, kwanini Niyonzima asijipige kifua bahati mbaya hata Azam wameangukia huku, hawajui na naamini hawajapata atakayeongeza makali ya Kipre.


Ndo maana huwezi kushangaa Yanga inakuwa na washambuliaji watano Mrwanda, Tegete, Javu, Tambwe na Sherman lakini haina mbadala wa Juma Abdul AMA Haruna Niyonzima. Kuna namna moja tu ambayo vilabu vya wenzetu vimeishi na kufanikiwa. Nayo ni kupitia usajili. Wekeza unavyojua, ingiza pesa utakavyo lakini usikosee kusajili. Hii ndo roho ya mafanikio yako kama unahitaji kuishi salama, hapa ndipo makocha kichwa kinapouma, hili ndilo eneo la msingi sana. Unamleta nani, atakaa muda gani, anaziba nafasi gani na kwanini yeye na sio mwingine. Haya ni mambo ambayo yanawafanya wamchukue mchezaji Fulani. Kuna sababu zinazofanya hata timu zenye usajili wa pesa ndogo kufanya vyema nalo limelala hapa, kusajili watu sahihi katika wakati sahihi na sehemu sahihi. Hawakurupuki, mahitaji ya vilabu wanayajua tangu ile filimbi ya mwisho ya mechi yao ya kwanza ya msimu, wanaanza mikakati ya kuipatia ufumbuzi.

Natamani yanga na wenzao waone hili, watambue hili. Mara chache sana Man united wakamsajiri mchezaji ili tu Man city wasimpate, hii inatokea tu pale ambapo unao wachezaji unaowahotaji na unaamua kumdhoofisha mpinzani ambaye anamhitaji Zaidi, kama Chelsea walivyowafanyia Liverpool kwa Mohamed Salah.

Nilikaa na kukumbuka namna yanga walivyoshindwa kupenya ngome ya Etoile Du Sahel pamoja na wao kuwa pungufu mechi ya pili, kulikuwa na jibu sahihi. Walikuwa na profeshino mmoja aliepotea siku hiyo Amis Tambwe, walimkosa Profeshino mmoja mwenye kariba ya Niyonzima kuisukuma timu, mwisho kabisa walikosa mtu sahihi ambaye angeweza kuleta miguu inayokaribiana na msuva uwanjani. Yanga walikuwa na kikosi cha kwanza pekee bila nyongeza nje. Kumpiga  Mazembe unahitaji Msuva wawili wanaokaribiana, unahitaji Sherman mwenye jicho la Tambwe na unamhitaji pacha wa Niyonzima. Hapo hata Makapu na Telela utawalinda na kuwa bora siku zote.

Hutokosa pumzi Niyonzima akiuzwa, huwezi kuwaza hata kumzuia Msuva kwenda kufanya majaribio. Tofauti na hapo utaendelea kushinda ubingwa wa vilabu ambavyo umefanana navyo tabia, yaani inakua kama kichaa anayejua kushika kalamu wakati vichaa wengine wamezubaa. Haimbadili kuwa kichaa, anakuwa na nafuu tu. Ni kama ambavyo Simba hawajawahi kumpata Mafisango tena, hawajawahi kupata mbadala wa mfumo na kikosi kilichowaonyesha ES SETIF kazi, lakini Setif walitoka pale na leo wao na Simba ni mlima Kilimanjaro na kichuguu fulani jirani na nyumba yetu. Kuna kiongozi aliwahi kukaririwa baada ya kuulizwa namna wanavyomsajili mchezaji akasema wanamuona kwenye YouTube halafu wanamuita kumfanyia majaribio kunakosekana tofauti ya uweledi Kati ya shabiki na kiongozi wa klabu ama benchi la ufundi.

Umefika muda yanga na wenzao wabandike picha ukutani tu, wautizame ule mfululizo au mtiririko wa wachezaji wao, wapi walishindwa kufunika na wapi walifanikiwa. Pengine hii inaweza kuwasaidia kujifunza na kukumbuka. Tofauti na hapo maandalizi ni muhimu ambayo mpaka leo ninavyoshika kalamu ya Makala hii sioni kama wamefanikiwa. Kama hutoniamini subiri CAF watoe ratiba.

Ahsanteni. By Nicasius Coutinho Suso

No comments

Powered by Blogger.