SOKA LA BONGO : KESSY NA NDUGUZO,  TAFUTENI WA KUWASHIKIA KALAMU KISHA MNUNUE SAA ZA MKONONI. 

Kessy akisaini kuichezea Simba

Hakuna rafiki mnafiki wa binadamu kama muda,  yeye huwa hasimami, harudi nyuma, hakuonei huruma na wala hasikilizi.  Ukipatia mtaenda sawa, ukikosea hausiki. Muda haumpi nafasi Tajiri kununua saa la ziada au nyongeza. Bahati mbaya Sana huyu ndiye rafiki ambaye huna namna na huna budi kuishi naye. Wanadamu wengi tumeshindwa kung'amua hili,  tunakosa kujiandaa kisha tunalaumu,  wanasiasa wanakosa uongozi bora na wanaishia kutumia vibaya rasilimali kumuwahi huyu,  balaa zaidi na kwa hawa wanamichezo hasa soka. Ukichelewa kidogo muda unakuacha mbali zaidi. Muda haujawahi kutoa fursa ya mpaka miaka 50 kwa mcheza soka, lakini wengi bado wanafanya utani nao. Viongozi kila siku wanawanyima Wapenda Soka fursa ya kufaidi mchezo kwa kushindwa kutizama muda. Na ndipo hapa hata wachezaji wa nyumbani wanaishi, hawajui wanacheza kwa sababu ipi, na hawajui kwanini wapo klabu fulani na nini wanahitaji katika muda huo. Kwao hawajawahi kuhesabu ni lini akili na misuli havitoendana, na lini magoti yataanza kugomea kazi za utumwa.

Kuna kitu katika maisha kinaitwa mkataba. Hii ni taaluma ambayo nchi nyingi za Afrika hatuifahamu, ni kitu muhimu zaidi ambacho wengi ukipuuzia. Bahati mbaya Sana na wenyewe ni tegemezi Sana kwenye muda. Huwezi kutenganisha muda na mkataba. Ni jukumu la muajiriwa kujua nini anataka katika muda fulani na wakati fulani. Kibaya zaidi ni katika kudadavua mkataba unasema nini. Kitendo cha wachezaji kuwa na mikataba ya mdomoni kuliko maandishi utaendelea kuwatafuna na kuua soka la Tanzania kwa ujumla. Umemsikia Kessy, anadai kakosa Nyumba kutoka kwa Simba,  unamkubuka Samata aligoma kwa sababu ya gari, na wengine wengi wa aina hii. Unakuwa unajiuliza je huwa hivi vitu wamevitaja kwenye mikataba?  Kwa ufuatiliaji wangu wa chini  wengi upewa ahadi kwa mdomo wakati mkataba ukiwa unasema mengine. Kuna matatizo mawili hapa. Kwanza ni elimu ndogo ya wachezaji wetu, pia uhuni wa viongozi wetu. Wachezaji hawaelewi nini wanatakiwa kufanya,  na pia viongozi hawawatakii mema wachezaji wetu kwa kutumia vibaya uelewa wao mdogo na kuwanyonya. Ikumbukwe hakuna sehemu unyonyaji unaruhusiwa na TFF imekosa nafasi ya kuwatetea Hawa kwa sababu nayo sio chombo huru (kimejaa viongozi watendaji wa vilabu hivi).


Umefika muda sasa soka la Tanzania liongozwe kiuweledi na kisasa zaidi,  wachezaji waijue thamani ya kalamu yao (sahihi). Kuajiri mwanasheria linaweza kuwa jukumu Zito lakini Pengine linawezekana kwa kuwa na chama cha soka cha wachezaji Tanzania ambapo kitasimamiwa na wanasheria kadhaa, na wachezaji wanachama watatakiwa kuwa na Ada ya kila mwezi kwa ajili ya kuwalipa hawa na watahusika na kusimamia mikataba yote, na kufafanua nini kimeandikwa katika kila mkataba ambao mchezaji atatakiwa kutia saini na klabu husika. Hawa watasimamia kuwashikia kalamu wachezaji (kusimamia wapi waweke sahihi na wapi wasiweke) na pia ni muda Sasa pia wachezaji watambue muda unahitaji nini. Soka la Sasa linataka nini na wachezaji wa kisasa wanaishije kulinda vipaji vyao.  Mwandishi Stephen King katika kitabu chake cha THE GREEN MILE aliwahi kusema katika maisha muda utakuja kuchukua kila kitu, uwe unataka au hutaki. Utachukua kipaji chako, utachukua nguvu zako na mwisho utaondoka n maisha yako. Inabidi wachezaji wajue hili, inabidi KESSY na wengine wajue hili na ndipo waupe muda thamani yake. Walishindwa kushika kalamu kwa usahihi Sasa watafute wakuwashikia kwa uangalifu, chama cha wachezaji soka inawezekana kuwepo, Walishindwa kuendana na muda Sasa wanunue saa za mkononi kuendana na kasi yake, maana kila muda wataona mshale wa saa unavyokwenda kasi.

 Ahsanteni By Nicasius Coutinho Suso

No comments

Powered by Blogger.