MAMBO KUMI NILIYOJIFUNZA BAADA YA ROBO FAINALI UEFA CHAMPIONS LEAGUE.
1. Kama Kuna mchezaji ambaye ameifikisha Barcelona hapo ilipo na haimbwi sana na hajawahi kuimbwa basi ni Sergio Busquets, baada ya Xavi Kuwa katika nyakati zake Za mwisho huyu Sasa hivi ndiye muamuzi wa namna pasi Za Barcelona zinavyopigwa, hata kusogea kwake na timu kumeongezeka tofauti na zamani.
2. Huitaji kikosi kikali ama wachezaji wazuri pekee kufika mbali UEFA champions League. Unahitaji mbinu Za kucheza mashindano haya. Blanc na PSG yake hawajawahi kujua kucheza haya mashindano, kama Manchester City tu. Kitu kinaitwa uwanja wa nyumbani ndio huwa silaha ya kwanza, hata Porto alifanikiwa hapa mpaka anafika Allianz Arena.
3. Tofauti kubwa Kati ya Pep Guardiola na makocha wengi ni Kuwa inabidi uanze kucheza na mbinu zake kabla ya kucheza na timu yake. Lopetegui alishindwa hapa. Lucescu pia, Kuna Pep Guardiola wawili duniani kwa sasa, anayecheza ugenini na Nyumbani. Huyu wa Nyumbani sio mzuri, amejaribu kuiboresha kiasi Tiktaka na kuongeza kasi katika Aina yao ya mchezo.
4. Sergio Ramos? Hata El Classico aje ajaribiwe pale katikati mwa uwanja, Kuna kipindi Mourinho alifanikiwa na Pepe lakini huyu Pepe hana utulivu na umakini wa kiungo. Kwa Ramos Ile namna yake ya kuusoma mchezo ndio kitu cha ajabu zaidi. Aliwatuliza sana Koke na Turan. Bahati mbaya kwa Diego Simeone lile Soka lake la kihuni analoliweka kati huyu analijua vyema, kwa kiasi kikubwa aliimeza staili ya Atletico Madrid. Ni mapema kusema lakini hii inaweza Kuwa njia mpya kwa Madrid kwenda kutetea kombe kupitia kwa huyu maana hata kushambuliwa kwao kumepungua.
5. Kale kaugonjwa kanaitwa Diego Costa bado kanautafuna ubongo wa Atletico Madrid. Mandzukic sio mzururaji mzuri kule mbele, na sio mhuni kule mbele Kuna ubabe fulani anaukosa . Huwezi kumtegemea sana mbele ya akina Pepe na Boateng au Mascherano. Ana tatizo pia la kutokuwaweka wenzake mchezoni na kuwa game decider (mwamuzi wa matokeo) lakini yule Griezman pia hajakomaa kucheza michezo mikubwa kwa kiwango chenye mwendelezo. Costa aliwapa kitu hiki. Aina yao ya mchezo ni Ile Ile tatizo ni moja tu, wamebaki na Upinde, huku mshale umepotea.
6. Kuna ule usemi unasema kwa mwendo huohuo Kobe hufika anapopataka. Kuna kitu kinaitwa UNDERDOG SYNDROME, kaugonjwa ka kuhisiwa wewe ni wa kawaida na mdogo kulinganishwa na wengine, hata atakaye pangiwa JUVENTUS Sasa hivi atakuwa anaiota fainali yenyewe kuliko atakavyoiwaza Juventus. Lakini hawa wana kikosi sahihi kabisa cha kutoa ushindani kwa mtu yoyote bado siwezi kuwaweka juu ya hawa wengine lakini kila nikiwaza mwendo wa Kobe napata shaka kama nilivyokuwa naandika siku zote, tunaweza kukutana nao fainali Berlin. Ukiwa na Pogba, Vidal, Pirlo, Marchisio, Tevez, wewe ni mshindani sio mshiriki.
7. Tofauti ya Barcelona hii na Ile ya Pep Guardiola ni Kuwa Ile ilikulazimisha kuachia mpira mapema kwa sababu walikaba kwa pamoja, hii inakukaba kwa uwepo wa Messi, Suarez na Neymar pale mbele. Hawa wote sio wakabaji, wala huwezi kuwatuma wakakabe, wanapomuongeza na Iniesta ambaye nguvu zinapungua wanakuwa na pungufu ya watu wanne wasiokaba kikamilifu. Unataka kuwafunga hawa, zuia eneo lao la kiungo ambalo kwa sasa linazuilika Kisha cheza mpira wa kukimbia, hawajawahi kuweza mchezo huo mpaka timu ya taifa. Ukicheza taratibu kama PSG wanafurahi zaidi.
8. Unajua kwanini Chicharito hapati nafasi Madrid? Jibu ni moja tu Cristiano Ronaldo. Tofauti yake na Benzema ni Kuwa ukiwa na Benzema anampa nafasi Cristiano kuingia vyema katika Ile Sita ya adui. Hii inatokana na uwezo wake mkubwa wa kutembea na mpira na kusaidia upatikanaji wa magoli na ndicho kitu Boss (Cristiano) anakipenda. Chicha yeye hana hayo, anajua sehemu yake sahihi ni katika sita, huko kwingine kuchoshana. Ndio maana dhidi ya Atletico Madrid kafanya majaribio mengi Zaidi kuelekea Langoni akiwa ndani ya sita kuliko mchezaji yoyote. Ronaldo hawezi kuishi maisha haya kwa mechi nne au tano mfululizo.
9. Kuna wakati unaweza kujiuliza Wenger anawaza nini. Tangu aondoke Viera amepata shida sana, lakini marafiki zake wa karibu wanayo bidhaa anayoweza kuipoka kwa urahisi zaidi. Bahati nzuri siku hizi hata yeye pochi yake inafunguka. Yule Kondogbia Ile jezi ya Arsenal, Wenger kaamua kuichelewesha, usishangae akija kupishana na Gundogan pale Dortmund. Kwa ufupi hii ndio Mali iliyowaweka Monaco mahala walipo sasa. Moja ya nguvu chache zinazokosekana EPL. Hata pale Liverpool nasikia yupo Allen, hawajawahi kuiwaza bidhaa hii. Matuidi, Pogba, Kondogbia, Deschamps ana kifua cha miaka mingi mbele pale timu ya taifa Ufaransa.
10. Kikubwa alichokuwa nacho Fc Porto ndicho alichokosa Monaco, na kizuri alichokitengeneza Monaco ndicho alichobakisha Fc Porto. Porto walijua kucheza vyema na kupata matokeo bora Nyumbani lakini ugenini hawakuwahi Kuwa wazuiaji wazuri achilia mbali rekodi yao, walikaribisha sana mashambulizi mara nyingi, upande wa Pili Monaco walijua kucheza ugenini huku Nyumbani walikuwa wanalala na miguu inakufa ganzi. Walipokutana na watu sahihi wamepata walichokikosa. Wakati Mwingine ni mwiba ndio unaweza kukumbusha umuhimu wa kiatu.
NB :
Uzuri wa Porto ni biashara tu. Kila mara wanaweza hapa na wale ndugu zao Benfica. Pale kwa kocha wao Lopetegui, na wale vijana Brahimi, Hector Herrera, Danilo, Jackson Martinez Kuna kama Pound 100 million. Halafu mwakani wanaenda tena Amerika ya kusini kuleta vitu. Unakumbuka Mourinho na vizazi vyake, AVB na watu wake akina Hulk na Falcao na James. Hii ndo tabia ya hawa, wanakula pesa ya UEFA mpaka mtoano wanakula pesa ya usajiri. Hawatopotea kama kina Psv na Ajax hawa.
Ahsanteni
By Nicasius Coutinho Suso
nnicasius@outlook
Insta: NicasNicho
No comments