ASANTENI BARCLAYS:KWENYE KIKAO CHENU CHA MWISHO NA VILABU MSIMU HUU NIPELEKEENI UJUMBE WANGU KWA WAFUATAO;
Ni msimu wa 23 tangu benki ya Barclays iwe mdhamini mkuu wa ligi kuu ya England. Kwanza napenda kuwashukuru sana Barclays kwa udhamini wao. Pia kuna kitu ningependa mnisaidie kukifikisha mahala husika. Wakati mnafanya mkutano wenu wa mwisho na vilabu vilivyoshiriki ligi kuu ya England msimu huu nawaombeni mjitahidi kuwaita pembeni wafuatao na kuwaambia yafuatayo huku mkiwa mmewapa kikombe cha kahawa kunogesha mazungumzo.
1:Anzeni na Manchester utd kwa kuongea na wachezaji hawa wawili, Radamel Falcao na Ange Di maria. Tena ikiwezekana Falcao awe wa kwanza. Kila nikimwangalia Falcao huwa nakumbuka ule msemo usemao kipya kinyemi ingawa kidonda.
Ujio wa Falcao Manchester united ulikuwa Furaha kubwa kwa mashabiki wa timu hiyo ila kwa sasa uwepo wake umekuwa kidonda kwao.Ni mshabiki gani hawajawahi kumlaumu Falcao? Nani hajawahi kutamani Falcao asiwepo msimu ujao? Ni wachache sana wanaotamani aendelee kuwepo mpaka msimu ujao. Juzi tulishuhudia Falcao akiifungia timu yake ya taifa ya Colombia magoli mawili.Hebu mkumbusheni ule msemo wa waingereza usemao "A guine-fowl not lay eggs on strange places"( kanga hazai ugenini) Namuomba apigane kweli kupingana na huo usemi. Magoli anayofunga nyumbani akiwa na timu ya taifa anatakiwa pia ayafunge ugenini akiwa na Manchester united. Mkumbusheni kuwa mimi ni mmoja wa watu wanaoamini kupitia miguu yake. Naamini akituliza akili yake baada ya muda mfupi atakuwa mfalme pale.
Kwa Di maria hapa kuna kichekesho.Waingereza walishawahi kusema "the Evil spirit of a man is a man" ( Ibilisi wa mtu ni mtu) .Mwanzoni mwa msimu mpaka juma la 20 la ligi Di maria alikuwa Mchezaji aliyekuwa akihusudiwa na mashabiki wa Manchester united.Ila michezo michache imefanya mashabiki wasahau Assists 10 za Di maria. Mwambieni Di maria atulie mkumbusheni jezi namba 7 ndo jezi aliyowahi kuivaa swahiba wake Cristiano Ronaldo, na ndo jezi aliyowahi kuivaa anayesemekana ndo mchezaji bora wa Uingereza wa wakati wote George Best, mkumbusheni alivaa mshambuliaji aliyefunga goli la kwanza la EPL Eric Cantona, bila kumsahau David Beckham. Mwambieni Di Maria afanye kitu kikubwa zaidi ya watangulizi wake hao.Mashabiki wanasubiri kuona vitu vizuri kutoka kwake kwa sababu ya jezi aliyovaa pia kwa sababu ya kiwango alichokionesha msimu uliopita.Ningekuwa mimi ndiye yeye ningetumia muda mwingi kuongea na ÖZIL NA RONALDO. Özil angenikumbusha alivyokuwa anashambuliwa na mashabiki na vyombo vya habari msimu uliopita na anavyoshangiliwa msimu huu.Ronaldo angenikumbusha umuhimu na ukubwa wa jezi namba 7 .
2:Wakati anatoka Feyenoord na kwenda St.Mary's stadium alikuta wachezaji Saba wa kikosi cha kwanza wameuzwa. Na alipoulizwa atafanya nini alijibu ataenda kufundisha uwanja mtupu na kuwataka mashabiki waje kushangilia.Huyu ni mtu mwingine ninayependa mumfikishie ujumbe wangu anaitwa "Ronald Koeman". Naweza kusema ni mfululizo wa mazao ya Ajax na Barcelona. Hivi ni kocha gani aliyepitia Ajax na Barcelona asiwe kocha mzuri? Ni msimu wake wa kwanza ila tayari mkononi ana tunzo mbili za kocha bora wa mwezi wa kwanza mwaka huu na mwezi wa tisa mwaka jana. Kaeni naye afu mwambieni kwamba akifanikisha kuwabakisha wachezaji waliopo na akaongeza ukubwa wa kikosi atakuwa mshindani halali wa Jose Mourinho msimu ujao.
3:Wakati 1993 dunia ikiwa kwenye homa ya mashindano ya kombe la dunia la 1994 nchini Marekani, mashindano yaliyomtoa chipukizi Marc Overmars mholanzi ambaye ameingia kwenye wachezaji bora 50 wa Arsenal wa wakati wote akiwa anashika namba 12.Kule uingereza kuna mama alikuwa anajiandaa kumtoa tumboni chipukizi hatari kwa sasa Harry Kane.Msimu wa jana alichezeshwa kwenye mchezo wa Capital one dhidi ya hull city aliifungia goli la kusawazisha ambalo ndo lilikuwa goli lake la kwanza kuifungia timu yake. Mechi yake ya kwanza ya ligi kuu dhidi ya sunderland alifunga goli moja kwenye ushindi wa magoli 5-1 .Mechi yake ya kwanza dhidi ya watani wao wa jadi Arsenal alifunga magoli mawili.Juzi mechi yake ya kwanza kwenye timu yake ya taifa alifunga goli lake la kwanza akiwa na jezi ya timu ya taifa na kutimiza magoli 30 msimu huu.Mwambieni anahitaji msimu mmoja zaidi kuwepo pale White hart line.Asije akatongozeka na noti za Real Madrid.Mara mia aende Manchester united akajifunze mengi kupitia Rooney, RVP na Falcao kuliko kwenda kufanywa bidhaa ya muda mfupi ya kuingiza hela pale R.Madrid.
4:Msimu huu inaonekana waingereza watajivunia sana .Usipotaka kumzungumzia Harry Kane kwa hasira zako za kukufunga lazima utamzungumzia Charlie Austin.Kwanini wakati kahawa ikishuka taratibu kooni mwake msimshauri aende timu nyingine. Mjaribuni kumshawishi aende angalau pale liverpool au aende pale Arsenal hakika atawasikia.Mkimaliza kwa huyo basi nendeni kwa mtoto ambaye kila nikimwangalia naiona jezi ya Manchester united mwilini mwake Dany Ings.Mwambieni alipo hapamfai.
5:Kuna mtu mkikaa naye mwambieni azidishe maombi ya De gea kugomea mkataba mpya na azidi kumwombea aende zake kwao,halafu yeye aende mahala pake.Msimu huu ametengeneza Clean sheet 13 zikiwa nyingi kuzidi kipa yeyote pale England. Sitaki kuzungumzia saves zake zilizomwingiza kwenye makipa 5 walio na saves nyingi msimu huu kwa sababu nitaonekana namsifia sana Fraser Forster. Mwambieni aanze kujipendekeza mapema kwa Manchester united maana hawatasumbuka kwenda mbali kutafuta mbadala wa De Gea kama ataondoka.
6:Mark Hughes na Alan pardew waambieni wabaki na timu zao.Wakati Mark Hughes anaichukua Stoke kutoka kwa Tony Pulis 2013 msimu wa mwaka 2013/2014 Alifanikiwa kuiingiza Stoke City kwenye Klabu kumi bora kwenye msimamo wa Ligi ikiwa ni mara ya kwanza kwa Stoke city.Msimu huu anauhakika mkubwa wa kuingia Kumi bora tena .Mwambieni abaki na ajitahidi kuongeza ukubwa wa kikosi msimu ujao tutamuona nafasi ya 6.
Kati ya makocha waingereza ambao ni bora basi Alan Pardew ni kocha bora na mzuri kitu alichokuwa anakosa ni ushirikiano tu.Pale Selhurst park ni pazuri kwake kuliko St.James Park.Mwombeni abaki pale na anijengee jiwe gumu litakalokuwa linawasumbua Kina chelsea na wenzake.
7:Nahisi huu ndo wakati wa Big sam kudhihirisha ukongwe wake pale Uingereza.Ni muda ambao tunahitaji kumuona akishindana na Arsenal,Chelsea,Manchester united , liverpool na Manchester city mwanzo hadi mwisho wa msimu.Mwambieni pumzi aliyoanza nayo msimu huu aanze nayo msimu ujao na isiishie katikati.
Ndo salamu zangu chache nawaombeni Barclays mzifikishe kwa wahusika.
Ahsanteni.
#Martin kiyumbi.

No comments